Habari Mseto

ANGLO LEASING: Githu na Wako waeleza mabilioni yalivyotoweka

June 22nd, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WALIOKUWA wanasheria wakuu Mabw Amos Wako na Prof Githu Muigai Alhamisi walieleza jinsi waliomba mataifa ya kigeni kusaidia Kenya kuchunguza kashfa ya Anglo-Leasing na kutambua zilikokuwa zimefichwa pesa zilizolipwa kampuni zilizohusika na sakata hiyo.

Bw Wako na Prof Muigai walifichua kuwa pesa hizo zilikuwa zimefichwa katika mataifa ya Uswizi , British Virgin Islands na Amerika.

Maafisa wakuu kutoka nchi hizo waliwasilisha ushahidi kwa Prof Muigai , alioupeana kwa tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) kuwachunguza wakuu serikalini na wenye makampuni hayo.

Bw Wako na Prof Githu waliotoa ushahidi mmoja baada ya mwingine walisema “ ushahidi ulipoletwa uchunguzi ulianza na washukiwa wakatiwa nguvuni na kufunguliwa mashtaka.”

“Niliomba Kenya isaidiwe na Jaji wa Mahakama ya Juu nchini Uswizi mwenye tajriba ya juu Dkt Mark Henzline aliyechunguza kampuni ya Anglo-Leasing na kuipa Kenya ushahidi. Pesa zilizokuwa zimelipwa kampuni hiyo Euro 5.2milioni (Sh506milioni) zilirudishwa nilipofutilia mbali kandarasi hiyo ya kuuzia idara ya polisi vifaa,” alisema Bw Wako.

Alitoa kama ushahidi wa vyeti 47 vya kandarasi tano kati ya Kenya na InfoTalent vya ununuzi wa vifaa vya usalama vya idara ya polisi.

Seneta wa Busia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu akiwa mahakamani Juni 21, 2018. Picha/ Richard Munguti

Wanasheria hawa wakuu walieleza jinsi waliandika mabarua ya kuomba Kenya isaidiwe kupokea ushahidi wa makampuni yaliyokuwa yanahusika kutoka ng’ambo.

Wawili hawa waliotoa ushahidi mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku walisema mataifa hayo ya kigeni yaliipa Kenya ushahidi kuhusu makampuni yaliyokuwa yamehusika katika sakata hiyo ya Sh3.8bilioni.

Wastaafu hawa walisema hayo walipotoa ushahidi dhidi ya wafanyabiashara watatu wa kimataifa Mabw Deepak Kamani, Rashmi Kamani na baba yao Chamanlal Kamani wanaoshtakiwa kwa kashfa hiyo pamoja na waliokuwa makatibu wakuu wizara za fedha na afisi ya rais Mabw David Onyonka na Dave Mwangi.

Watano hawa wamekanusha kufanya njama za kuilaghai Serikali zaidi ya Euros 40milioni (Sh3.8bilioni) kupitia mradi wa kununulia idara ya polisi vifaa vya mawasiliano na maabara almaarufu E-Corps.

“Nilifutilia mbali kandarasi iliyokuwa imetiwa saini kati ya Kenya na kampuni ya kimataifa ya InfoTalent iliyomilikiwa na familia ya Kamani,” alisema Bw Wako.

Bw Wako alisema afisi yake wakati huo mwaka wa 2003 iliombwa na aliyekuwa katibu Afisi ya Rais Bw Mwangi isome na kuidhinisha kandarasi iliyokuwa imetayarishwa kati ya Serikali na InfoTalent inayomilikiwa na familia hiyo ya Kamani  yenye afisi nchini Geneva , Uswizi.

“Bw Mwangi aliomba afisi yangu isome na kutoa ushauri wa kisheria kuhusu kandarasi kati ya Kenya na InfoTalent,” alisema Bw Wako.

Kandarasi hiyo, Bw Wako alisema ilisomwa na mawakili wa Serikali Bw D Achapa na Bi Roselyn Amadi wote wa kitengo utengenezaji kandarasi kati ya Kenya na Nchi za Kigeni.

Kandarasi hiyo ilisomwa na Bi Amadi na kuirudisha OP irekebiswe.

“ Ilirudishwa tena na Amadi akaikosoa kisha akarudisha OP,” alisema Bw Wako.

Hatimaye ilitiwa saini na aliyekuwa Waziri wa Fedha marehemu David Mwiraria , aliyekuwa Katibu mkuu Wizara ya hazina Bw Joseph Magari, Bw Mwangi  na InfoTalent.

Kesi itaendelea Agosti 20 2018 mashahidi wanane watakapotoa ushahidi.