Kimataifa

Ang'olewa macho kwa kutamani dume lingine Facebook

May 6th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMUME kutoka Uingereza amepatikana na makosa kumng’oa mpenzi wake macho, kumchapa kisha kumfungia katika nyumba, baada yake ‘kulike’ picha za mtu mwingine kwenye mtandao wa Facebook.

Mahakama ilimpata Danny Bridges, wa miaka 35 na makosa hayo wiki iliyopita, kufuatia kosa hilo alilofanyia eneo la Whitstable, Kent, Uingereza.

Alidaiwa kumnyonga na kumpiga ngumi mpenzi wake huyo, kabla ya kuingiza vidole vyake katika macho ya mpenzi wake huyo, hali iliyomfanya mwanamke huyo kuhofia kuwa macho yake yangeng’oka.

Ili marafiki na watu wa familia wasione majeraha machoni mwa mpenzi wake, Bridges alimfungia katika nyumba kati ya Oktoba 31 na Novemba 2, 2018.

Lakini mwanamke huyo alimtumia rafikiye ujumbe mfupi kutafuta msaada, na rafikiye huyo akapigia polisi ambao waliwasili na wakamkamata Bridges.

Habari za polisi zilionyesha kuwa mwanamke huyo alidai mwanamume huyo alikasirika na akaanza kumvamia wakati aliona akipendezwa na ‘kulike’ machapisho ya marafiki zake. “Alikuwa akinikemea na kuniingilia kwa ‘kulike’ machapisho ya watu Facebook.

Kila ngumi aliyonipiga nakumbuka tu nikiona giza, hadi akaniingiza vidole machoni,” akasema mwanamke huyo kwa polisi.

Lakini mdhulumiwa alipofika kortini alieleza korti kuwa alipata majeraha alipoanguka wakati alipokuwa chooni, kinyume na habari zake kwa polisi.

Aidha, mdhulumiwa alieleza korti kuwa majeraha aliyokuwa nayo shingoni, kwenye mikono na miguuni yalitokana na kufanya ngono na Bridges.

Jaji alikataa kumuamini na kuamua kuwa mwanamume huyo ni hatari, akisema “mwanamke yeyote atakayejihsisha na mwanamume huyo siku za usoni yuko hatarini.”