Habari Mseto

Ang'olewa paa la nyumba kwa kuchelewa kulipa kodi ya Aprili

April 20th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MPANGAJI mmoja katika mtaa wa Kariobangi South, Nairobi Jumatatu aling’olewa paa la nyumba kwa kuchelewa kulipa kodi ya mwezi huu wa Apili, huku visa vya kama hivi vikiendelea kuripotiwa katika maeneo kadha nchini.

Hii ni kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayosababishwa na athari za mlipuko wa ugonjwa hatari wa Covid-19.

Bw Jackson Ng’ang’a Mwangi, 35, alisema mwanawe wa kiume wa mmiliki wa nyumba hiyo alitekeleza kitendo hicho ilhali amekuwa akimlipa kodi kwa miaka miwili iliyopita bila kuchelewa. Hulipa kodi ya Sh6,000 kila mwezi kwa nyumba ya vyumba viwili.

Baada ya mabati kuondolewa hapa, mwanya umejitokeza katika paa la chumba cha jirani ambapo mvua yaweza kumnyeshea akiwa ndani. Picha/ Charles Wasonga

“Juzi nilimwambia kijana wa mwenye nyumba kwamba anipe muda nitafute pesa nitamlipa lakini akasisitiza kuwa sharti nimpe pesa hizo leo (Jumatatu) la sivyo nihame. Na leo asubuhi nilipoondokwa kwenda kutafuta riziki jirani alinipigia simu kwamba amekuja na kung’oa paa la nyumba,” akaambia Taifa Leo Dijitali.

Bw Mwangi ambaye anaendesha biashara ya kuuza VCD za nyimbo za injili katika mtaa wa Huruma alisema amelemewa kulipa kodi ya nyumba kutokana na kuzorota kwa biashara ambako kumechangiwa na janga la corona.

“Sijakataa kulipa, lakini biashara sio nzuri wakati huu kwa sababu wateja wangu wengi wameathirika na makali ya corona,” akaeleza.

Huu ni utovu wa utu kumng’olea mpangaji paa kwa kuchelewa kulipa kodi. Baadhi ya malandilodi huwaongezea wapangaji muda wa kulipa. Picha/ Charles Wasonga

Mwanawe mmliki wa nyumba hiyo anayejulikana kama Mwash, alisisitiza kuwa sharti Mwangi alipe kodi ya mwezi huu au ahame.

“Huyu jamaa lazima alipe pesa. Mbona analalamika ilhali wapangaji wengine wamelipa. Kwani wao hutoa wapi pesa?” Mwash alisema, tulipomfikia kwa njia ya simu.

Bw Mwangi aliandikisha taarifa kwa kituo cha polisi cha Kinyago katika mtaa wa Dandora Phase 1.

Na katika kitongoji cha Chokaa katika eneobunge la Embakasi ya Kati, Bi Jackline Akinyi aling’olewa paa na milango kwa kutolipa kodi ya mwezi huu ya Sh2,000.

Akinyi, ambaye ni mjane huendesha biashara ya nguo za mitumba katika mtaa wa Umoja 1 ni mama wa watoto wawili.

Jackson Ng’ang’a Mwangi aliyeng’olewa paa na mwanawe landilodi kwa kutolipa kodi ya Aprili ya Sh6000. Picha/ Charles Wasonga

Katika kisa kingine sawa na visa hivi, Bi Caroline Achieng alibomolewa paa na milango ya nyumba katika mtaa wa Nyalenda, Kisumu kutokana na malimbikizi ya kodi ya Sh2,400.

“Niliamka na kupata fundi akiondoa mabati kwenye paa. Aliniambia kuwa amepewa maagizo na mwenye nyumba ang’oe sehemu ya paa kwa sababu sijalipa kodi ya miezi miwili,” Bi Achieng ambaye ni mjane alinukuliwa akisema.

Aliongeza kuwa juhudi zake za kutaka apewe muda zaidi na mwenye nyumba, kwa jina Nyakano, ziliambulia patupu.

Visa hivi vinaripotiwa wakati ambapo Bunge la Seneti linajadili mswada ambao unalenga kuwashurutisha wamiliki wa nyumba za makazi wasiwafurushe wapangaji watakaolemewa kulipa kodi wakati huu wa janga la corona.

Mswada huo ambao umedhaminiwa na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja unawataka wenye nyumba kuelewana na wapangaji kama hao ili walipwe baada ya janga hili kudhibitiwa.