Habari Mseto

Anne Thumbi atoa masharti kabla mazishi ya Ken Okoth

August 2nd, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

HALI ya vuta nikuvute inazidi kushuhudiwa kati ya familia ya marehemu mbunge wa Kibra Ken Okoth na mpenziwe Anne Thumbi huku utata unaozingira mazishi ya kiongozi huyo ukichukua mkondo mpya kufuatia masharti yaliyotolewa.

Mnamo Alhamisi, Agosti 1, 2019, Thumbi ambaye ni diwani maalumu katika bunge la Kaunti ya Nairobi na anayedaiwa kuwa mpenzi wa siri wa marehemu Okoth, alitoa masharti matatu anayotaka yatimizwe kabla ya kuidhinishwa mazishi.

Diwani huyo anataka familia ya marehemu imlipe kiasi fulani cha hela cha kugharimia masomo ya mtoto wao wa kiume waliozaa pamoja na vilevile apatiwe matokeo ya uchunguzi wa DNA.

Isitoshe, katika kesi hiyo ambayo ameiwasilisha kwa niaba ya mwanawe, ambapo amewashtaki mamake Okoth, Angelina Okoth, mjane Monica Okoth, na Lee Funeral Home kama mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu, Thumbi anataka ahusishwe pamoja na mwanawe katika mipango ya mazishi.

Mnamo Alhamisi, Hakimu Grace Mmasi alimpa diwani huyo kibali cha korti cha kusimamisha ama kuteketezwa au kuzikwa kwa mwili wa Okoth hadi kesi hiyo iliyotengewa tarehe ya kusikizwa Agosti 9, 2019, itakaposikizwa na uamuzi kutolewa.

“Idhini ya muda itolewe na inatolewa sasa ikiwazuia wawili hao ama wao binafsi, watumishi wao au maajenti dhidi ya kufanya mazishi, shughuli za mazishi, uteketezaji au namna nyingine yoyote ya kuuzika mwili wa Okoth,” ulisema uamuzi wa Hakimu Mmasi.

Awali, kupitia wakili wake Elias Mokaya, Thumbi alikuwa amelalamikia dhidi ya familia hiyo kumtenga katika mipango ya mazishi ya Okoth. Alihoji kwamba anataka mwanawe kutambuliwa na familia hiyo akisema ana wasiwasi kuhusu mustakabali wake wa kupata elimu.

Aidha, anataka Lee Funeral Home na mochari nyingine zozote kuzuiwa kutoa mwili wa mwanasiasa huyo hadi matokeo ya DNA yatakapotolewa mbele ya wataalamu kutoka pande zote.

Mnamo Alhamisi, Gavana wa Nairobi Mike Sonko alizua tumbojoto miongoni mwa waombolezaji wakati wa ibada ya mazishi ya Okoth alipopasua mbarika kuhusu uhusiano wa kimapenzi kati ya marehemu na Thumbi ambao matokeo yake ni mtoto wa kiume.

“Mimi ni shahidi. Nitakuwa nimemkosea Ken kwa kunyamazia haya kwa sababu ninajua ukweli. Walikuwa wakichumbiana na hata mara ya mwisho walikuwa Ufaransa pamoja. Ninamhurumia Monica, ninajua ni mjane kipindi hiki kigumu lakini acheni niseme ukweli,” Sonko alisema huku baadhi ya watu wakimshangilia.