Makala

ANNETTE MUCHITI: Filamu ina raha lakini changamoto zipo

June 15th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

KILA mja hujipa matumaini ambapo huwa ni hali ya kutarajia. Ni katika hali ya kutumainia na kuvumilia ambapo anaaminia nyota yake itang’aa na kutinga upeo wa mwigizaji wa kimataifa miaka ijayo.

Anasema hajapiga hatua kubwa katika maigizo lakini ana imani atafika mbali. Annette Muchiti Emali maarufu kama Shimuli ama Minayo alianza kujituma katika maigizo miaka kumi iliyopita.

”Bila kujipigia debe ninalenga kukaza buti nihakikishe nimetinga hadhi ya waigizaji mahiri duniani kama Caryn Elaine Johnson mzawa wa Marekani maarufu kama Whooppi Goldberg.

Elaine aliye mtangazaji, mwigizaji, mwandishi wa vitabu pia mchekeshaji anajivunia kushiriki filamu kama ‘Sister Act,’ ‘The Color Purple,’ ‘Ghost,’ na ‘Corrina, Corrina,’ kati ya zingine. Kisura huyu mwenye umri wa miaka 30 anasema kuwa alipata motisha zaidi katika sekta ya maigizo baada ya kuteuliwa kuwania tuzo katika hafla ya Riverwood Awards 2016 kitengo cha Best Supporting Actress).

KALASHA AWARDS

Demu huyu aliteuliwa kuwania tuzo hiyo baada ya kushiriki filamu kwa jina ‘Kijakazi Chizi,’ iliyozalishwa na kundi la Shoeback Production.

”Kusema kweli uteuzi huo ulichangia pakubwa kupata nafasi kuigiza filamu nyingi tu,” alisema na kuongeza kuwa alivutiwa na masuala ya maigizo baada ya kutazama filamu kwa jina Sarafina enzi hizo akiwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi mwaka 2002. Kadhalika anasema anatamani sana kushinda tuzo kama ‘Calasha Awards’ kati ya zingine miaka ijayo.

JACKIE APPIAH

Kipusa huyu ambaye hufanya kazi na Shoeback Production anajivunia kushiriki filamu nyingi tu ambapo baadhi yazo zimefaulu kupata mpenyo na kupeperushwa kupitia runinga tofauti hapa nchini. Baadhi ya filamu ambazo zimepata nafasi kuonyesha kwenye runinga ni kama ‘Kijakazi Chizi(Startimes Swahili),’ ‘Auntie Boss (NTV),’ ‘Creative Totos (Brandplus TV),’ ‘Sweet ride Movie (K24),’ na ‘Anikwa (Switch TV). Pia ameshiriki filamu zingine kama ‘Miheso,’ Kahawa Tungu,’ ‘Varshita,’ na ”Majirani,’ kati ya zingine.

Barani Afrika anatamani sana kufanya kazi na waigizaji kama Jackie Appiah (Ghana) na Auntie Ezekiel (Tanzania) waliogiza filamu kama ‘The King is mine,’ na ‘Mrembo Kikojozi,’ mtawalia. Hapa Kenya anasema angependa kufanya kazi na waigizaji kama Brenda Wairimu pia Celestine Gachuki walioigiza filamu kama ‘Mali’ na ‘Selina,’ mtawalia.

MILIMA NA MABONDE

Katika uigizaji wanawake hupitia changamoto sio haba. Anadai nyakati zingine hufanya kazi na kutolipwa na wahusika hali ambayo huchangia wengi wao kuvunjika moyo na kuwazia kusepa.

”Kando na hayo nimejikuta kwenye wakati mgumu maana maprodyuza wengine hupenda kunishusha hadhi na kuniomba tuwe wapenzi ili kunipa ajira,” anasema na kuongeza kuwa suala hilo limechangia anyimwe nafasi za ajira mara kadhaa.

Anakiri kwamba hukosefu wa soko ndiyo hutatiza tasnia ya uigizaji nchini. Kipusa huyu anashauri wenzake watie bidii wala wasivunjika moyo wanaposaka ajira ya uigizaji pia wamwaminie Mungu.