Michezo

Ansu Fati afungia Uhispania dhidi ya Ukraine na kuvunja rekodi kadhaa

September 8th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI chipukizi wa Barcelona, Ansu Fati, alitangaza makali yake kwenye soka ya kimataifa mnamo Jumapili kwa kuweka rekodi ya kuwa mfungaji wa umri mdogo zaidi katika historia ya timu ya taifa ya Uhispania.

Fowadi huyo alifunga bao na kusaidia mabingwa hao wa zamani wa Kombe la Dunia kusajili ushindi wa 4-0 dhidi ya Ukraine katika mechi ya UEFA Nations League uwanjani Alfredo di Stefano, Uhispania.

Fati, ambaye ni mzawa wa Guinea-Bissau, alipata uraia wa Uhispania mwaka 2019 licha ya kwamba alihamia katika taifa hilo akiwa na umri wa miaka saba pekee. Anakuwa mwanasoka mchanga zaidi kuwahi kuwajibishwa na Uhispania katika kipindi cha miaka 84.

Kwa kufunga bao dhidi ya Ukraine mnamo Jumapili akiwa na umri wa miaka 17 na siku 311, Fati alivunja rekodi ya ya miaka 95 ya Juan Errazquin aliyewafungia Uhispania mabao matatu dhidi ya Uswisi akiwa na umri wa miaka 18 na siku 344 pekee mnamo 1925.

“Pindi nilipopata ofa ya kubadilisha uraia, niliwasiliana na familia yangu iliyonipa idhini ya kufanya hivyo. Nawashukuru sana wazazi na walezi wangu kwa msaada ambao umeniwezesha kukabiliana vilivyo na changamoto mbalimbali hadi kufikia sasa kitaaluma,” akasema.

Fati anajivunia pia rekodi za kuwa mfungaji wa umri mdogo zaidi katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) akivalia jezi za Barcelona ambao wamenyanyua taji la UEFA mara tano na la La Liga mara 26.

Mnamo Jumapili, Fati alichangia penalti iliyofungwa na nahodha Sergio Ramos dhidi ya Ukraine na akaweka historia nyingine ya kuwa mchezaji wa pili mchanga zaidi kuwahi kuwajibishwa katika kivumbi cha Nations League.

Ethan Ampadu aliyechezea Wales dhidi ya Bulgaria mapema Jumapili, ndiye mwanasoka wa kwanza kuwahi kunogesha kivumbi cha Nations League akiwa na umri wa miaka 17 na siku 357 pekee.

Aliwajibishwa mwaka jana katika gozi lililowakutanisha Wales na Jamhuri ya Ireland.

Ramos ambaye alifunga mabao mawili katika gozi hilo, sasa amepachika wavuni magoli 10 katika mechi 15 zilizopita za kimataifa. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34, amefungia Uhispania jumla ya mabao 23 katika historia, na anasalia na goli moja pekee kufikia rekodi ya aliyekuwa nguli wa kikosi hicho, Alfredo di Stefano.

Bao jingine la Uhispania katika mechi hiyo iliyokuwa ya kwanza kwa beki Eric Garcia wa Manchester City kuwajibishwa, lilifumwa wavuni na sajili mpya wa Manchester City, Ferran Torres.