Antonio Conte kuendelea kuwa kocha wa Tottenham msimu ujao

Antonio Conte kuendelea kuwa kocha wa Tottenham msimu ujao

Na MASHIRIKA

ANTONIO Conte, 52, atasalia kuwa kocha wa Tottenham Hotspur msimu ujao.

Kulikuwa na tetesi kwamba Mwitaliano huyo angebanduka kambini mwa Spurs mwishoni mwa msimu huu licha ya waajiri wake kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika muhula ujao wa 2022-23.

Hata hivyo, taarifa kwamba usimamizi wa Spurs unalenga kumwaga sokoni kima cha Sh23.4 bilioni kwa minajili ya kusaidia kikosi hicho kujisuka upya msimu ujao ni kiini cha Conte kufikiria upya kuhusu mpango wa kuondoka.

Conte aliyeagana na Inter Milan mwishoni mwa msimu uliopita wa 2020-21, alikutana na mkurugenzi wa soka wa Spurs, Fabio Paratici, nchini Italia mnamo Mei 27, 2022 na kumpa hakikisho la kuendelea kudhibiti mikoba ya Spurs.

Kinachosubiriwa sasa ni kuona iwapo mkufunzi huyo wa zamani wa Chelsea atatia saini mkataba mpya kambini mwa Spurs ikizingatiwa kwamba kandarasi yake ya sasa na kikosi hicho inatamatika mnamo 2023 huku akiwa radhi kurefusha mkataba huo kwa miezi 12 zaidi.

Conte alipokezwa mikoba ya Spurs mnamo Novemba 2021 na akaongoza klabu hiyo kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu katika nafasi ya nne na hivyo kufuzu kwa soka ya UEFA.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Karua ahofia kura kurudiwa kama 2017

Nations League: Italia kualika Uingereza uwanjani San Siro...

T L