Kimataifa

Anusurika kifo akipiga 'selfie' na chatu

June 20th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

JALPAIGURI, INDIA

AFISA wa kutunza wanyamapori alinusurika kifo wakati joka aina ya chatu alilokuwa ameokoa lilipomkaba shingoni alipotaka kupiga naye picha.

Ripoti zinasema afisa huyo aliyetambuliwa kama Sanjoy Dutta aliongoza kikosi cha maafisa waliookoa joka hilo katika msitu ulio Wilaya ya Jalpaiguri, India.

Video ilisambazwa mitandaoni ilimwonyesha akiwa ameshikilia joka hilo na kuliweka begani huku akizungukwa na wenzake wakitaka kupiga picha ya kumbukumbu.

Lakini punde joka hilo lenye urefu wa futi kumi lilianza kumkaba shingoni ikalazimu wenzake waingilie kati kumwokoa.

Kwa kawaida chatu anapokaba mtu mwilini huwa anamzuia kuvuta hewa na hivyo basi kufariki.

Umati uliokuwepo ambao awali ulikuwa ukishangilia ujasiri a maafisa hao, ulianza kupiga nduru kwa hofu.

Hata hivyo, wenzake walifanikiwa kumvuruta chatu huyo hadi akamwondokea shingoni. Baadaye walimwachilia huru akatorokea vichakani.

-Imekusanywa na Valentine Obara