Habari Mseto

Anusurika kifo katika ajali ya Ijumaa Thika Superhighway

November 23rd, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MTU mmoja alinusurika kifo Ijumaa baada ya gari lake kupoteza mwelekeo na kugonga reli katika barabara ya Thika Superhighway.

Ajali hiyo iliyotokea eneo la Clayworks, kilomita moja hivi kutoka mtaa wa Githurai, ilihusisha gari la mmiliki binafsi na lililoendeshwa na mwanamke.

Lilikuwa katika leni ya kasi kutoka jijini Nairobi.

Kulingana na walioshuhudia, huenda gurudumu lilipasuka na gari likapoteza mwelekeo ambapo liligonga nguzo za kando ya barabara na kung’oa vyuma.

Vyuma vinne viling’olewa na nguzo hiyo kukatika.

“Inaonekana lilikuwa kwa mwendo wa kasi, kiasi cha kung’oa vyuma hivyo na kujaribu kuvuka barabara ya kuelekea jijini Nairobi,” mmoja wa walioshuhudia akaambia Taifa Leo.

Maafisa wa Mamlaka ya Barabara Kuu Nchini (KeNHA) walifika ili kutathmini kilichosababisha ajali hiyo.

Mwanamke huyo aliyenusurika, hakuweza kuzungumza kwa wakati huo.

Sehemu ya mbele ya gari ilionekana kuharibika kupita kiasi, ingawa kioo cha kuzuia upepo hakikuvunjika.

“Kilichomuokoa ni kujifunga mkanda. Iwapo hangetekeleza hilo, kasi aliyokuwa ingemsababishia madhara,” akasema dereva mmoja wa matatu.

Afisa wa idara ya trafiki na aliyebana jina lake aliambia mtandao huu kwamba uchunguzi umeanzishwa.

“Tunahimiza madereva na watumizi wa barabara wawe waangalifu. Kasi ni hatari, na huua,” akaonya.

Mapema Novemba 2019 ajali nyingine ilitokea eneo la Githurai.

Ilihusisha magari manne; basi, gari aina ya probox, pickup na gari la binafsi.

Thika Superhighway si geni kwa visa vya ajali, vingi vikihusishwa na uendeshaji wa magari kwa mwendo wa kasi, baadhi ya madereva wakiingia barabarani wakiwa walevi na ubadilishaji wa leni pasi uangalifu.

Endapo gurudumu la gari limepasuka ukiwa kwa mwendo wa kasi, unashauriwa kushikilia usukani na kulidhibiti, ukisalia katika leni ulioko. Usikanyage breki mara moja, kwani huenda likabingiria.

Washa mataa ya dharura ili kufahamisha walio nyuma yako. Litaanza kupunguza mwendo, na huo ndio wakati unashauriwa kukanyaga breki, hususan kasi ikiwa chini ya kilomita 50 kwa saa.

Toa vifaa vya dharura na kuviweka mita chache nyuma ya gari. Ili kuondoa msongamano barabarani, tafuta gari likuvute kwa unyororo au mekanike akurekebishie.

Maafisa wa KeNHA na trafiki hata hivyo huwa barabarani kwa ajili ya kuangazia masuala ya aina hiyo.