Kimataifa

Aoa mtoto wa miaka 16, awataka wazazi wake kumpa pesa za kumlea

May 15th, 2019 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU
 
WAZAZI wa msichana tineja kutoka nchini Uingereza ambaye alitoroka nyumbani kwenda kuolewa na mwanamume mzee wameachwa kuduwaa, baada ya kupokea barua ya kuwataka kulipia gharama ya kukimu maisha ya mwanao.
 
Claire Milliner mwenye umri wa miaka 42 na Martin Chambers wa miaka 47 walishangaa baada ya binti yao wa miaka 16 kutorokea Sctotland kuoana na Thomas Arnold wa miaka 27, Desemba mwaka jana.
 
Wawili hao walijuana katika mitandao ya kijamii na wakasafiri hadi eneo la Gretna Green, Scotland ambapo watoto wa miaka 16 wanaruhusiwa kufunga ndoa, bila idhini ya wazazi.
 
Hata hivyo, wazazi hao walishangaa wakati walipokea barua kutoka idara ya ulezi wa watoto, ikiwataka walipe zaidi ya Sh300,000 kugharamia malezi ya mtoto wao.
 
Wazazi hao wanaamini kuwa barua hiyo ni baada ya aliyemuoa binti yao kuweka maombi hayo.
 
“Sikuamini, bado alikuwa shule hata alipomuoa na sasa ana ushupavu wa kudai malipo ya kumlea. Si ni mkewe,” Bi Milliner akasemma.
 
Lakini idara ya kusimamia masuala ya watoto ilieleza Mashirika ya habari kuwa inaamini barua hiyo ilitumwa kimakosa.
 
“Watu hawawezi kudai malipo ya ulezi wa watoto kwa mtu ambaye ameolewa kwani kisheria mtu huyo ni mtu mzima,” akasema msemaji wa idara hiyo.
 
Watu wengi husafiri hadi Gretna Green kufungia ndoa huko kwani sheria za huko hazina mahitaji mengi, uwepo wa mashahidi wawili tu ukiwa hitaji kuu, ila umri wa wahusika huwa si jambo lenye uzito.