Habari Mseto

AP aliyetoroshwa kituo cha polisi na wenzake akamatwa upya

December 17th, 2018 1 min read

Na HILLARY KIMUYU

AFISA wa polisi wa utawala ambaye alitoroshwa kutoka kwa kituo cha polisi katika Kaunti ya Mandera na wenzake, amekamatwa tena na kupelekwa Nairobi kizuizini.

Kulingana na ripoti za polisi, maafisa 14 waliovamia kituo cha polisi cha Mandera ili kumtorosha mwenzao, wameagizwa kwenda Nairobi ili wachukuliwe hatua za kinidhamu.

“Ni lazima hatua zitachukuliwa kikamilifu. Kile walichofanya hakikustahili na hakiwezi kupuuzwa bila adhabu,” akasema afisa mmoja wa ngazi za juu anayefahamu kuhusu kisa hicho.

Alhamisi iliyopita usiku, maafisa 14 walivamia kituo cha polisi cha Mandera ambacho ndicho makao makuu ya polisi mjini Mandera,, wakamtorosha Koplo Richard Githaka Karanja.

Maafisa hao kutoka katika kambi ya polisi wa utawala ya Mandera Kapendo, walienda kituoni humo kwa miguu wakiwa wamevaa sare kamili, wakafyatua risasi hewani huku wakitaka mwenzao aachiliwe huru.

Baada ya kumwondoa kizuizini, walifyatua risasi nne hewani na kutorokea kambi ya Kapendo ambayo iko karibu kilomita tano kutoka kituoni humo.

Kikosi cha polisi kilitumwa Mandera kumkamata upya, kisha wengine 14 wakapelekwa Ijumaa kushikilia mahala pa watakaoadhibiwa.