Habari Mseto

Apatikana na hatia ya kumuua mpenzi miaka minane iliyopita

April 3rd, 2019 1 min read

TITUS OMINDE na CEDRICK KHAYEKA

MAHAKAMA Kuu mjini Eldoret imempata mwanaume mmoja na hatia ya kumuua mchumba wake miaka minane iliyopita.

Jaji Olga Sewe alimpata Bw Andrew Kihugwa na hatia ya kumuua Sydney Khaisha mnamo Novemba 12 mwaka wa 2011 katika kijiji cha Kaptogongeni kaunti ya Nandi.

Wakati wa mkasa huo, mwendazake alikuwa kwenye mzozo na mshukiwa kuhusu uhusiano wao wa kimapenzi.

Mwendeshaji mashtaka aliiambia mahakama kuwa, mwendazake alikuwa akielekea dukani wakati alikumbana na mauti yake.

Mshukiwa alikuwa amejihami na kisu. Wawili hao waliongea kwa muda karibu na kanisa moja mahali ambapo Khaisha alipatikana baadaye amelala chini na kisu hicho kikiwa kando yake.

Familia ya marehemu ilielekea mahali pa mkasa baada ya kuarifiwa na kumpeleka hospitalini alikoaga akipokea matibabu. Kisu hicho kilichochukuliwa na polisi kilitumiwa kama ushahidi katika kesi hiyo.

“Baada ya kupokea malalamishi, mahakama itamsomea mshukiwa mashtaka ili aweze kupata nafasi ya kujitetea,” alisema jaji Sewe.

Kulikuwa na idadi ya mashahidi saba katika kesi hiyo.

Jaji Sewe alisema kuwa ametosheka na ushahidi uliowasilishwa mbele ya mahakama ikidhibitisha kuwa mshukiwa alihusika katika mauaji ya mwendazake.

“Nimetosheka na ushahidi uliowasilishwa mbele yangu, mshukiwa anatarajiwa kujitetea kwa mashtaka ya mauaji dhidi yake kulingana na kifungo cha 306(2) cha utaratibu wa mashtaka ya jinai.” Jaji Sewe aliamua.

Mshtakiwa anatarajiwa kufika mahakamani tarehe 26 mwezi huu ilia pate kujitetea.