Habari Mseto

Apatwa na hatia ya kumdunga mpenzi visu 16 kwa kunyimwa uroda

November 30th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME aliyemuua mpenziwe kwa kunyimwa tendo la ndoa alipomdunga kisu mara kumi na sita katika sehemu nyeti  na tumboni Alhamisi alipatikana na hatia ya kuua.

Jaji Roselyn Korir alimpata na hatia James Mulu Mulewa ya kumuua Mercy Ngari katika mtaa wa Mathare,  kaunti ya Nairobi mnamo Feburuari 27, 2012.

Mshtakiwa alimteremsha Mercy suruali ya ndani na kumdunga kisu sehemu zake nyeti, tumboni , mapaja  na makalio mara 16,” alisema Jaji Korir.

“Upande wa mashtaka umethibitisha ni wewe ulimua Mercy. Ulimwandama kutoka steji hadi kwa nyumba ya mama yake. Ukafunga mlango kisha ukamshinda nguvu alipokunyima ngono na ukasababisha kifo chake kwa kumdunga kisu,” Jaji Korir.

Akijitetea Mulu alisema , marehemu alikuwa akimsingizia alikuwa na urafiki na wasichana wengine lakini ushahidi huo wake ukafutiliwa mbali na jaji akisema ,” hicho ni kisingizio tu kuficha uhalifu mbaya aliotenda.”.

“Ni  Mercy ambaye angelihudhika kwa kusikia mpenziwe Mulu anawachumbia wasichana wengine,” alisema Jaji Korir akiongeza, “haya ni madai ya kujaribu kumlimbikizia marehemu mizigo.”

“Mshtakiwa alijifungia ndani ya nyumba ya mama wa Mercy na kujaribu kumbaka,” alisema Jaji Korir.

Jaji alisema mshtakiwa alimlaza marehemu kwenye kitanda cha mamaye na kujaribu kumnajisi.

Korti ilisema mshtakiwa aliposhindwa kutekeleza tendo la ngono kwa nguvu, alitwaa kisu na kumdunga Mercy mara 16.

“Mshtakiwa alidunga nyeti ya Mercy mara sita. Mara sita alimdunga tumboni , mapajani mara mbili na kwenye makalio mara mbili,” alisema Jaji Korir.

Mahakama ilisema mshtakiwa alikataa kufungua mlango hata baada ya majirani wa marehemu kumsihi.

Polisi walijulishwa kisa hicho na kuombwa wafike nyumbani kwa marehemu kwa vile kulikuwa na kisa cha mauaji.

“Polisi walipofika walimpata mshtakiwa amejifungia ndani ya nyumba akiwa na marehemu,” alisema mshtakiwa.

Mahakama ilisema polisi walipofika walimshawishi mshtakiwa kisha akafungua na kumpata Mercy amelala kitandani akiwa mfu.

Korti ilisema damu ilikuwa imetapakaa kwote chumbani.

Alisema mashahidi waliofika mahakamani walisema mshtakiwa na marehemu walikuwa wapenzi.

“Hii mahakama imekupata na hatia ya kumuua Mercy kwa kumdunga kisu mara 16,” alisema Jaji Korir.

Alirudishwa rumande hadi wiki ijayo atakapofika mahakamani kujitetea na kuhukumiwa.