Kimataifa

Apatwa na kifafa cha ghafla baada ya kuumwa na nyoka 'aliyefufuka'

June 12th, 2018 1 min read

MASHIRIKA na VALENTINE OBARA

TEXAS, AMERIKA

MWANAMUME aliyemkata nyoka mara mbili na kumuua alishtuka wakati kichwa cha nyoka huyo ‘kilipofufuka’ kumuuma na kumfanya apate majeraha mabaya na kifafa cha ghafla.

Kulingana na mashirika ya habari, mwanamume huyo alikuwa ameona nyoka aina ya ‘rattle snake’ mwenye urefu wa futi nne kwenye bustani kisha akamkata mara mbili kwa kutumia sepetu.

Wakati alipookota kichwa cha nyoka huyo ili akakitupe ndipo aliumwa bila kutarajia, na sumu ya nyoka ikamwingia mwilini.

Ripoti zinasema wakati huo huo alianza kupoteza uwezo wa kuona huku akivuja damu na akitetemeka mwili mzima ikabidi apelekwe hospitalini kwa helikopta.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya wanyama, kuna aina ya nyoka ambao huendelea kuwa na uhai katika sehemu ya juu ya mwili kwa muda kwa sababu ubongo wao huchukua muda mrefu kuangamia hasa kama bado kichwa kimeshikana na shingo, na hivyo basi watu huhiotajika kujihadhari hata baada ya kukata nyoka mara mbili.