Habari Mseto

Apigwa dhamana ya Sh500,000 kwa kuiba jogoo

January 17th, 2019 1 min read

Na TITUS OMINDE

MWANAMUME wa miaka 24 ambaye alikabiliwa na mashtaka ya wizi wa jogoo wa Sh600 aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini wa kiasi sawa katika mahakama moja mjini Eldoret.

Mahakama iliambiwa kuwa Silas Opollo Etyang pamoja na watu wengine ambao hawakuwa kortini walimvamia na kumwibia Bi Nora Liseche, jogoo wake kabla ya kumuacha na majeraha mwilini mwake.

Stakabadhi za mashtaka kortini zilielezea kuwa tukio hilo lilitokea mnamo Januari 10 mwaka huu katika kijiji cha Maragusi kaunti ndogo ya Lugari.

 

NMshtakiwa alikamatwa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Lugari baada ya tukio hilo kuripotiwa.

Hata hivyo alikana mashtaka dhidi yake.

Hakimu mkuu mwandamizi wa Eldoret Bw Harrison Barasa aliamuru mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi 500,000.

Kesi hiyo itasikizwa mnamo Januari 28.

Mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana mwanaume wa umri sawa na mshtakiwa aliuliwa na umma katika Kijiji cha Lukhome kaunti ndogo ya Kiminini kaunti ya Trans Nzoia kwa madai ya kumwibia jirani wake kuku wa kima cha Sh400.