Habari Mseto

Apigwa kama mbwa koko baada ya kufumaniwa akichuna ngozi mke wa jirani

June 6th, 2018 1 min read

Na Tobbie Wekesa 

Butere, Mumias

WENYEJI wa hapa walipata fursa ya kutazama sinema ya bure baada ya polo kupewa kichapo alipofumaniwa na mashemeji akichovya asali ya jirani yake.

Kulingana na mdokezi, kulikuwepo na madai kwamba polo aliacha familia yake ikiteseka na kutekwa na mke wa jirani yake.

Mashemeji wake walikuwa wamemuonya aache tabia hiyo na kumtunza dada yao lakini hakukoma.

Siku ya kioja, jamaa na mashemeji walikutana kwa mama pima.

Inasemekana baada ya kunywa, polo aliamua kuondoka na kuwaacha mashemeji zake.Penyenye zinasema mashemeji waliamua kumfuata polo hadi kwa mpango wake wa kando.

“Ulituambia unaenda wapi? Hapa ni kwako? Leo utatujua,” mashemeji waliapa. Pombe ilimwisha polo mwilini.

“Huna adabu hata kidogo. Kwako ni pale. Una mke mzuri tu. Kwa nini unaleta aibu kama hii. Leo ni leo,” mashemeji walimkaripia polo huku wakiingia ndani ya nyumba.

Habari zilizotufikia zinasema walimzaba polo makofi na kumvuta hadi kwake. Kulingana na mdokezi, polo aliomba msamaha huku akiahidi kutorudia ufuska tena. “Dada yetu ameteseka sana. Mara hii utaishi kwa masharti yetu,” mashemeji walimuonya polo.