Michezo

Apigwa marufuku mechi 27 kwa kukwaruza kichuna wake kifuani

September 14th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

Mchezaji wa klabu ya magongo ya Nashville Predators nchini Marekani, Austin Watson amepigwa marufuku mechi 27 kwa kosa la kushambulia mpenzi wake mwezi Juni katika eneo la kuegesha gari katika kituo cha kutoa huduma ya petroli.

Kamati ya nidhamu ya ligi hiyo ya NHL ilitangaza Septemba 12, 2018 marufuku hiyo dhidi ya mchezaji huyo Muamerika mwenye umri wa miaka 26, ambaye hakukubali ama kukataa kosa hilo.

Chama cha wachezaji wa ligi hiyo kilisema kwamba kitakata rufaa kuhusu marufuku hiyo.

Kulingana na polisi nchini Marekani, Watson alionekana akibishana na kipusa huyo ndani ya gari katika eneo la Franklin jimboni Tennessee. Idara ya Polisi ilisema kipusa huyo alionekana akitokwa na damu mguuni na alikuwa na mikwaruzo kifuani.