Wakazi wampiga mwendawazimu wakidai ni mchawi

Wakazi wampiga mwendawazimu wakidai ni mchawi

NA CHARLES ONGADI

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 33 alipokezwa kichapo cha mwaka  na umati kwa tuhuma za uchawi katika kijiji cha Majaoni, Bamburi, Mombasa siku ya Jumanne asubuhi.

Lakini kulingana na baadhi ya wakazi , mama huyo wala hakuwa mchawi kama ilivyodaiwa. Taifa Leo Dijitali ilithibitisha kuwa alikuwa mwendawazimu.

Mwanamke huyo aliyetambuliwa kama Bi Agnes Wakesho, alipigwa na umati wa wananchi wenye hasira baada ya kudaiwa kupatikana ndani ya chumba cha mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

“Mwanamke huyu alifumaniwa ndani ya chumba cha watoto usiku wa manane na haikuweza kuleleweka jinsi alivyoingia humo ndani na baada ya kuonekana akatoroka kupitia paa la nyumba,” akadai mmoja kati ya wanakijiji hiki ambaye hakutaka kutajwa jina.

Aidha, kulingana na mlinzi mmoja wa usiku aliyekuwa karibu na eneo la tukio ni kwamba alimshuhudia mama huyu akiwa juu ya paa la nyumba mwendo wa saa kumi na moja alfajiri.

“Umati ulifika mara moja na kuanza kumrushia mawe akiwa juu ya paa ya nyumba huku wakimtuhumu kuwa mchawi,” akasema mlinzi huyo wa usiku.

Hata hivyo, baada ya mwanamke huyo kupitia kipigo kikali ndipo alijitokeza mwanamume aliyetambuliwa kama Patrick Mutembei aliyesema  alikuwa ni mke wake ila ana matatizo ya kiakili.

Maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Bamburi, Kiasuni wakimwondoa mtuhumiwa wa uchawi Bi Agnes Wakesho baada ya kupigwa na umati katika kijiji cha Majaoni. PICHA CHARLES ONGADI

Kulingana na mlinzi wa kanisa la New Life, mwanamke huyo aliletwa na familia yake katika kanisa hilo kuombewa lakini alitoroka usiku wa manane .

Bw Kahindi Kalume aliiambia Taifa Leo Dijitali kwamba mwanamke huyo amekuwa akichuuza nguo katika mtaa wa Mkoroshoni na Majaoni lakini alionekana kuchanganganyikiwa tu kiakili huku akipinga dhana potovu kwamba alikuwa ni mchawi.

Naibu chifu wa Bamburi Bw Jeremiah Machache aliyefika mara moja katika eneo la tukio aliwaonya wananchi kuhusu uamuzi wa kuchukua sheria mikononi mwao.

“Jamii inahitajika kufuata sheria ya nchi na kuondoa dhana ambazo zimepitwa na wakati kuhusu uchawi, huenda mama huyu alirukwa na akili na hali hii inaweza kuzua hali yoyote kutokana na nguvu za giza ,” akasema Bw Machache.

Maafisa kutoka kituo cha polisi cha Bamburi walifika mara moja na kumkimbiza mama huyu katika kituo cha matibabu kuokoa maisha yake.

Visa vya watu kuuliwa kutokana na tuhuma za kiuchawi zimeongezeka sana jimbo la Pwani hasa zikiwalenga wazee wenye mvi.

You can share this post!

IEBC yaomba radhi kwa kuita BBI ‘Burning Bridges...

FAUSTINE NGILA: Teknolojia itatusaidia pakubwa mwaka wa 2021