HabariSiasa

Apigwa risasi akiingia Ikulu 'kumuua' Uhuru

June 12th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) anauguza majeraha ya risasi aliyopigwa alipojaribu kuvamia Ikulu kwa kile alikuwa amesema ni juhudi za kumuua Rais Uhuru Kenyatta, Jumanne.

Akiwa amejihami kwa kisu, Brian Kibet Bera, wa miaka 25, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tano anayesomea uhandisi wa mashine chuoni JKUAT, alikuwa amepanga kumvamia Rais kwa muda lakini vitisho vyake vikachukuliwa kama mzaha.

Msemaji wa Ikulu, Bi Kanze Dena alithibitisha kuwa Bera alivamia Ikulu mnamo Jumatatu jioni kwa kuruka ukuta, na akapigwa risasi bega la kushoto na walinzi, alipokataa kusimama na badala yake akawatishia kwa kisu.

Tangu Ijumaa iliyopita, Bera alikuwa akitoa vitisho dhidi ya Rais Kenyatta kwenye akaunti yake ya mtandao wa Facebook.

Alitoa vitisho vya mwisho Jumapili saa tatu na dakika 15 usiku ambapo alisema: “Kesho (Jumatatu) nitavamia Ikulu. Mungu amenituma kutekeleza hukumu dhidi ya kila mwizi na washirika wa wezi.”

Akinukuu sura mbalimbali za Biblia zinazokemea wizi, mshukiwa huyo alilalamika kwamba Rais Kenyatta ameongoza utawala wa unyanyasaji ambao umesababisha umaskini mkubwa kwa Wakenya wa kawaida.

“Nilimwandikia Rais Kenyatta barua mnamo Januari 2019 ili aniruhusu mimi na jeshi langu (watu maskini walionyanyaswa na wasio na makao) twende kuishi mapangoni katika Mbuga ya Kitaifa ya Mlima Elgon. Hiyo ni ardhi ambako mababu zangu waliishi. Hajanijibu!” akadai, mnamo Jumapili.

Alitangaza vita dhidi ya Rais na sekta ya mabenki anayodai ndiyo inashawishi maamuzi ya utawala wa Jubilee, na akapuuzilia mbali baadhi ya watu walioeleza hofu kwamba huenda ana matatizo ya kiakili.

Kulingana naye, alitia bidii mno katika shule ya msingi kwa kuamka saa tisa usiku kusoma hadi akapata alama 407 kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE), ambazo zilimwezesha kujiunga na Shule ya Upili ya Nairobi School.

Alisema katika shule ya upili pia alitia bidii na hivyo basi ni heri akawe mtumwa Ethiopia kuliko kuishi Kenya kwani bidii yake haimsaidii.

Licha ya kuwa inafahamika wazi Ikulu ni mojawapo ya maeneo yenye ulinzi mkali zaidi Kenya, mwanafunzi huyo alieleza kwamba ana hakika hatauawa, na pia vita alivyoanzisha sio vya waoga.

“Ninakatiza masomo. Elimu ni mateso na ushetani ambao unanifanya nisonge mbali na Mungu,” akasema.

Aliongeza: “Sababu yangu kuandika haya yote bila uoga ni kwa sababu ninajua hawawezi kunikamata. Na endapo watanikamata, wenzangu watawaua.”

Fununu zimekuwa zikienea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mipango ya mapinduzi ya umma dhidi ya Serikali ya Jubilee inayolaumiwa kwa kusababisha hali ya maisha kuwa ngumu, huku wizi wa mali ya umma ukiongezeka kwa manufaa ya walio madarakani na mabwenyenye.

Mapema mwezi uliopita, mwanaharakati mashuhuri Boniface Mwangi alikamatwa na maafisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) waliodai anapanga kupindua serikali.

Alipoachiliwa baada ya kuandikisha taarifa na kufuatia malalamishi makali kutoka kwa wananchi, Bw Mwangi alisema: “Wakenya wana hasira, njaa na hawana pesa. Wanahisi kusimama dhidi ya utawala mbaya na ufisadi na serikali inaogopa kitakachotokea. Wananchi si wapumbavu, wanajua nani ni mporaji na watamwandama, wakati huo ukifika hakuna atakayewazuia.”

Kamanda wa Polisi eneo la Kilimani, Bw Michael Muchiri alisema Bera atahojiwa kabla ya kushtakiwa.