Habari Mseto

Apinga DNA yake kutumiwa katika kesi ya Willy Kimani

October 26th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MMOJA wa washukiwa watano wanaoshtakiwa kwa mauaji ya wakili Willy Kimani miaka minne iliyopita Jumatatu alipinga kuwasilishwa kwa ushahidi wa ripoti ya DNA iliyochukuliwa kutoka kwake bila idhini.

Bw Peter Ngugi alimweleza Jaji Jessie Lesiit kwamba polisi walikandamiza haki zake kwa kuchukua sampuli kutoka kwa mdomo wake kupelekwa kupimwa na mtaalamu katika maabara ya serikali.

Bw Ngugi alisema sampuli hizo zilikuwa zinapimwa kubaini ikiwa ndiye alitupa kipande cha sigara aliyovuta mahala wakili Kimani, mteja wake Josephat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri waliuliwa Juni 23 2016.

Wakili Kelvin Michuki anayemwakilisha Bw Ngugi, aliyekuwa kachero katika kikosi cha polisi alilalamika kwamba Inspekta Robert Owino alikaidi sheria alipompeleka mshtakiwa huyo kutoa sampuli katika maabara ya serikali bila idhini yake.

Bw Michuki alisema mshukiwa yeyote uulizwa idhini anapotakiwa kutoa sampuli kupimwa ndipo matokeo yatumike kama ushahidi katika kesi inayomkabili.

Wakili huyo alinukuu sheria nambari 122 (A) na 122 (C) (1) kuwasilisha ombi lake. Pia alisema kifungu nambari 24 cha katiba kufafanua tetezi zake.

“Kuchukua sampuli za mshukiwa bila idhini yake ni kukandamiza haki zake kwa mujibu wa kifungu nambari 24 (1) cha Katiba,” alisema wakili huyo.

Wakili huyo alisema utaratibu ulitotumika kuchukua sampuli hizo haufai hata. Mahakama ilielezwa Insp Owino hakumkabidhi mshtakiwa nakala aliyoandika kuomba achukue sampuli za kupimwa.

Sampuli hiyo ilichukuliwa mnamo Agosti 29 2016 wakati Ngugi alichukuliwa kutoka seli alikokuwa anazuiliwa kisha akapelekwa afisi za uchunguzi wa jinai kisha akapelekwa kwa mtaalam katika maabara ya serikali na wakati huo wote hakuarifiwa kuhusu sampuli hizo.

Lakini naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma DDPP Nicholas Mutuku aliomba korti itupilie mbali ombi la Bw Ngugi akisema sampuli zilichukuliwa kwa njia inayotambulikana kisheria.

Bw Mutuku alimkabidhi Jaji Lesiit ushahidi ulitayarishwa na Mkemia wa Serikali Bi Lucy Wachira na Insp Owino.

Wakili wa familia za wahasiriwa Bw Fred Ojiambo aliomba korti ikubali ripoti hiyo. Kesi itaendelea Jumanne