Habari Mseto

Aponea kifo baada la kutumbukia ndani ya Mto Ngong akivuta mkokoteni

January 2nd, 2019 1 min read

Na SAMMY KIMATU

MWANAMUME aliyekuwa akivuta mkokoteni akisafirishia mteja bidhaa katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba, South B, Kaunti ya Nairobi aliponea kifo kwa tundu la sindano baada ya kutumbukia ndani ya mto Ngong Jumatano.

Walioshuhudia walisema mwanamume huyo alikuwa akibebea mteja bidhaa za nyumba alipooamua kuhama kutoka mtaa hupo hadi wa Mukuru-Hazina.

“Alikuwa akitoka Kaiyaba akielekea Hazina lakini mkokoteni ulikuwa umebeba sana. Alipofika kwa mlima, alishindwa kupanda na ndipo mkokoteni ulirudi nyuma kwa kasi na kutumbukia ndani ya mto,” Bi Cynthia akasema.

Kisanga hicho kilivutia wakazi wengi waliofurika. Ni tukio lililotokea katika daraja la Kaiyaba/Hazina.

Katika eneo la kisa kulionekana godoro, meza, nguo, vyombo vya jikoni miongoni mwa vitu vingine.

Wasamaria wema waliingia ndani ya mto huo na wakamsaidia jamaa kumtoa nje ya maji na kisha wakatoa mkokoteni pia.

Mwenye kuhamishwa aliyeonekana kushtushwa na kisanga alidinda kuongea na wanahabari.