Habari Mseto

Aponea kunyongwa kwa kumuua mwanawe

April 25th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MWANAMUME aliyehukumiwa kunyongwa kwa kumuua mwanawe miaka tisa iliyopita, alipata afueni baada ya Mahakama ya Rufaa kubatilisha hukumu hiyo na kumfunga jela miaka 20 kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Naftaly Mukundi Waweru atatumikia miaka tisa jela pekee baada ya Majaji wa Mahakama ya Rufaa Philip Waki, Mohamed Warsame na Gatembu Kairu kuamua kwamba hukumu hiyo itahesabiwa kuanzia Mei 29 2009 aliposhtakiwa kwa mara ya kwanza kwa kosa hilo.

Majaji walikubaliana na wakili wa mshtakiwa Celyne Odembo kwamba Jaji F. N. Muchemi, hakuzingatia ushahidi wote uliotolewa mahakamani alipomhukumu Mukundi kutiwa kitanzi kwa kumuua mwanawe Fedrick Waweru Mukundi aliyekuwa na umri wa miaka 12.

Jaji Muchemi alikuwa amempata na hatia ya kutenda kosa hilo katika kijiji cha Rusingiti, Kiambu  mnamo Mei 11 2009.

Wakibatilisha hukumu hiyo, majaji wa Mahakama ya Rufaa walisema haikuthibitishwa Mukundi alikuwa amepanga kumuua mwanawe japo alikiri kwamba alikuwa amempiga akishuku alikuwa ameiba nyundo yake.

“Kwa upande wetu, tunafikiri kwamba ushahidi uliopo hauwezi kutumiwa kuthibitisha kesi ya mauaji. Ushahidi wote wa upande wa mashtaka unaonyesha kuwa kifo cha kusikitisha cha mtoto huyo hakikuwa kimepangwa. Kwa msingi huu, mshtakiwa angepatiwa jambo ambalo mahakama haikufanya,” walisema majaji katika hukumu yao.

Walisema japo ripoti ya mtaalamu wa kuchunguza maiti ilionyesha marehemu alikuwa na majeraha kichwani, haikuthibitishwa ni mshtakiwa aliyeyasababisha.

“Kwa hivyo, tunabatilisha hukumu ya kunyongwa na kuibadilisha na kuua bila kukusudia na kumhukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kuanzia Mei 21 2009 aliposhtakiwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu,” majaji waliamua.