Dondoo

Apoteza demu kwa kimya cha siku mbili

August 13th, 2018 1 min read

Na Leah Makena

Kirigara, Chogoria

JAMAA wa hapa alilazimika kurudi mawindoni baada ya kutemwa na mpenzi wake alipokosa kumvutia waya kwa muda wa siku mbili.

Inaarifiwa kuwa polo alikuwa na mazoea ya kumpigia kidosho simu kila siku ila mambo yakabadilika alipoingia mitini kwa muda wa siku mbili baada ya wawili hao kutofautiana.

Kulingana na mdokezi, wawili hao walikosa kuelewana kuhusu harusi yao kidosho alipoanza kulalamika kuwa jamaa alikuwa akisita ilhali aliwakataa majamaa wengi waliotaka kumuoa.

Inasemekana jamaa hakufanikiwa kumshawishi kidosho kuwa alitaka muda wa kujipanga kabla ya kumuoa kwani kidosho alidai kuwa jamaa alitaka tu kuchovya asali kisha atoweke na kumuacha.

Baada ya kukosa kuelewana kuhusu harusi ndipo simu za jamaa zilipopungua, jambo lililomchoma kidosho roho na kuhisi kuwa alikuwa akichezewa.

Hapo ndipo aliamua kumgeukia mmoja wa machali waliokuwa wakimmezea mate na akamsahau polo.

Siku mbili baada ya kumtema ndipo jamaa alifika kwa kidosho na kugundua alikuwa amepigwa teke na mrembo kunyakuliwa na kalameni mwingine .

Licha ya kujaribu kumbembeleza mrembo na kuomba radhi, polo aliachwa mataani kwani mrembo alikuwa amejipa shughuli.

Duru zasema kuwa polo alidai simu yake ilikwa imepotea ila mwanadada akadinda kukubaliana naye akisema polo alijua namba ya simu na hivyo angetumia simu yoyote kumpasha kuhusu kupotea kwa simu yake.

“Sitakubali uniharibie muda wangu kwa sababu sitaki kuwa mzee nikiwa kwa baba yangu. Kama uko na muda wa kuharibu chezea vipusa wengine ila sio mimi,” kidosho alimueleza.

“Ninajua ulikuwa unawaza iwapo utaendelea kunichumbia au la, ila nishakupa jawabu. Endelea kujipa muda utaoa wale ambao hawana haraka ya maisha.”