Michezo

APs Bomet yalenga kutua ligi ya NSL msimu ujao

March 19th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KOCHA wa Maafande wa APs Bomet Sebastian Owino amesema wamepania kuonyesha ubabe wao kwa kupiga shughuli safi ili kufukuzia tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Supa Ligi ya Taifa (NSL) msimu ujao.

Alisema haya baada ya wachana nyavu hao kutoka nguvu sawa bao 1-1 na Egerton University FC kwenye mechi ya Kundi B Ligi ya Taifa Daraja ya Pili iliyoandaliwa Silibwet Stadium.

”Mechi za msimu huu siyo rahisi tayari zimeashiria kuwepo ushindani mkali ambapo lazima tujitume ili tuwapiku mahasimu wetu,” alisema na kuongeza wanataka kumaliza kileleni ili kutuzwa tiketi ya kusonga mbele.

Chini ya nahodha Ramadhan Ali, APs Bomet ilitangulia kufunga kupitia Chrispinus Ikibasa huku Derrick Lang’at akisawazishia Egerton University.

Nayo Raiply FC iliandikisha ushindi wa pili msimu huu baada ya kucheza mechi kumi ilipodunga Poror Mote bao 1-0. Kwenye matokeo hayo, matumaini ya Zoo Youth kuzoa alama tatu ugenini yaligonga ukuta iliporandwa mabao 2-1 na Kisumu Allstars.

Kwenye jedwali, Zoo Youth inaongoza kwa alama 21 sawa na Bungoma Superstars tofauti ikiwa idadi ya mabao. Nayo Vihiga Bullets imetinga tatu bora kwa kufikisha pointi 20 tatu mbele ya APs Bomet.