Arama asukumwa jela miezi sita

Arama asukumwa jela miezi sita

NA RICHARD MUNGUTI

MATUMAINI ya Mbunge wa Nakuru Mjini Magharibi Samuel Arama yametokomea kabisa baada ya kusukumwa jela miezi sita kwa ufisadi.

Wiki iliyopita jopo la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) liliamuru Arama asiidhinishwe kuwania kiti cha ubunge Nakuru Mjini Magharibi kwa sababu ya ufisadi.

Arama alitozwa faini ya Sh1,560,000 kwa kujipatia ardhi ya mtu mwingine kwa njia ya udanganyifu.

Arama alihukumiwa pamoja na Wasajili watano wa mashamba katika Wizara ya Ardhi kaunti ya Nakuru John Mburu Mwaura, Daniel Kimoru Nyantika, Charles Onyambu Birundu na Kennedy Begi Onkoba.

Wote watano walihukumiwa na hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Victor Wakumile.

Bw Wakumilie alisema watano hao walikula njama za kumlaghai Bw Ahmed Muhammad Nisar shamba lake lenye thamani ya Sh60 milioni lililoko jijini Nakuru.

Akipitisha hukumu, Bw Wakumile alisema washtakiwa wote ni watu walio na ushawishi katika serikali ikitiliwa maanani Arama ni Mbunge na mtunzi wa sheria.

“Washtakiwa wote ni watu walio na ushahiwishi mkubwa katika jamii. Mwaura, Nyantika ,Birundu na Onkoba ni mawakili wanaojua sheria barabara ilhali Arama ni Mbunge na mtunzi wa sheria. Wanajua athari za kuvunja sheria,” alisema Bw Wakumile.

Hakimu alisema washtakiwa hao walitekeleza makosa mabaya lakini shamba lilirudishiwa mwenyewe Bw Nisar alipolalamika kwa polisi.

Arama alipatikana na hatia ya kujipatia hati ya umiliki wa shamba hilo akidai aliinunua kutoka kwa Yusuf Mustafa Ratemo kwa bei ya Sh60 milioni.

Kwa ujumla washtakiwa hao watalipa faini ya Sh4,160,000 ama watumike kifungo cha miezi sita.

  • Tags

You can share this post!

Uingereza wakomoa Italia na kufuzu kwa fainali ya Euro U-19...

Wajackoyah kutumia bangi, nyoka na mbwa kukwamua Kenya...

T L