Arati akana madai ya uhasama na Seneta Onyonka

Arati akana madai ya uhasama na Seneta Onyonka

NA WYCLIFFE NYABERI

GAVANA wa Kisii, Bw Simba Arati, amepuuzilia mbali madai kwamba ametofautiana na Seneta wa kaunti hiyo Bw Richard Onyonka, miezi kadha baada ya uchaguzi mkuu.

Gavana na Seneta wake walikuwa katika kambi moja kuelekea uchaguzi wa Agosti 9 na walifanyiana kampeni za dhati wakitafuta uongozi.

Baada ya kampeni kali zilizojaa msisimko, walipigiwa kura kwa wingi, baada ya kupata idadi kubwa ya kura kutoka takribani kila koo za jamii ya Abagusii.

Lakini katika wiki za hivi majuzi, kumekuwa na minong’ono kuwa hawazungumzi kwa sauti moja na mbwembwe na usuhuba waliokuwa wakionyesha hadharani wakati wa kampeni umegeuka kuwa “hewa moto.”

Dalili za madai ya wawili hao kutofautiana zilidhihirika Alhamisi wiki jana wakati gavana Arati, kwenye hafla ya kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani katika uwanja wa Michezo wa Nyanturago, eneo bunge la Nyaribari Chache, alidai kuwa baadhi ya watu ambao hakuwataja walikuwa wameanza kumpaka tope kwa sababu alikuwa amesimama kidete kulinda rasilimali za umma dhidi ya ubadhirifu.

“Kelele mnazozisikia ni kwa sababu baadhi ya watu waliokuwa wamejipanga tena wameona ni vigumu kula pesa zenu. Sasa wana nia ya kunipiga vita kisiasa kwa sababu nimewazuia kuchukua pesa zenu,” gavana Arati alisema.

Mjadala kuhusu uhusiano wa gavana na seneta ukiendelea katika kundi moja la mtandao wa kijamii, seneta Onyonka alidai kwamba baadhi ya watu walikuwa wakimsema vibaya kwamba kama si gavana Arati, hangekishinda kiti cha useneta.

You can share this post!

TAHARIRI: Si busara serikali kurudisha ada za benki kwa...

Polisi wanasa washukiwa wawili wa ujambazi

T L