Habari za Kitaifa

Mahakama yaagiza Arati na Nyaribo kushauriana kumaliza mzozo wa Keroka

March 12th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

MAHAKAMA imewaagiza magavana Simba Arati (Kisii) na Amos Nyaribo (Nyamira) kufanya mazungumzo ndani ya siku 21 kuhusu utoaji huduma usiotatizika katika mji wa Keroka.

Makamanda wa polisi kutoka sehemu hizo pia wameamrishwa kuweka mikakati itakayowahakikisha wafanyabiashara usalama katika mji huo unaozozaniwa na kaunti hizo.

Maagizo hayo yalitolewa na Jaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Nyamira Mugo Kamau anayesikiliza kesi kuhusu mgogoro wa mpaka wa Keroka.

“Keroka inamilikiwa na watu wa jamii moja. Sioni sababu yao kupigana kwa sababu ya mvutano kuhusu mipaka. Natoa agizo kwa magavana wote wawili washauriane kujaribu kutatua tofauti zozote,” jaji Kamau akasema Jumanne.

Jaji huyo alikuwa amemtaka gavana Arati kufika mbele ya Mahakama baada ya diwani wa Rigoma Nyambega Gisesa, kumshtaki kuwa alikuwa amekiuka uamuzi wa korti ulioweka bayana mipaka ya kaunti hizo katika mji huo.

Bw Arati alishtakiwa pamoja na Kaimu Katibu katika Serikali ya Kaunti ya Kisii Robert Ombasa na walitii agizo la mahakama.

Kwa muda mrefu, kaunti za Kisii na Nyamira zimekuwa zikizozania mji huo unaokua kwa kasi.

Kutafuta suluhu kuhusu hali hiyo, Bw Gisesa (ambaye wadi yake ya Rigoma iko Kaunti ya Nyamira) aliyoyomea mahakamani na kuiomba iweke wazi mahali mpaka huo uliko.

Aidha, Jaji Kamau kwenye uamuzi wa awali alikuwa ametoa uamuzi wake kuhusu mpaka wa Keroka. Uamuzi huo ulitegemea pakubwa ramani za masoroveya kutoka kwa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kulingana na ramani hizo, sehemu ambazo awali zilikuwa zinachukuliwa kuwa ziko Kisii, zilionekana kuwa ni za Nyamira.

Hivyo wakati wa kutoa uamuzi, jaji Kamau alisema serikali za kaunti hizo zinafaa kuzingatia kulikowekwa vigingi vya kuonyesha mpaka huo.

Jaji Kamau alisisitiza kuwa hilo pia linafaa kufuatwa katika ukusanyaji wa kodi na mapato mengine kutoka kwa wafanyabiashara.

Kesi hiyo itatajwa tena April 30, 2024.

Mnamo Machi 3, 2024, kulitokea vurumai katika mji huo unaokua kwa kasi baada ya maafisa wa kutekeleza amri za Kaunti ya Nyamira kujaribu kuwapokonya wafanyabiashara miavuli.

Miavuli hiyo ya rangi ya chungwa, ilikuwa imepeanwa na Bw Arati kuwakinga wafanyabiashara na hali mbaya ya hewa.

Aidha Bw Arati alichapisha picha na jina lake katika miavuli hiyo.

Kilichokera maafisa wa Nyamira ni kwamba kiongozi huyo wa Kisii katika kupena miavuli aliwakabidhi baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la chini ambalo katika uamuzi wa majuzi kortini, lilipatikana kuwa la Nyamira.

Kwa kuwa mji huo wa Keroka umegawanywa katikati na barabara kuu ya Kisii-Sotik, wafanyabiashara wa upande mwingine ambao hawakupewa miavuli hiyo walionekana mayatima, hali ambayo ilitajwa kwamba ilichochea moto vurumai hizo.

Ilibidi maafisa wa polisi kutumwa hapo kutuliza joto lililokuwa likipanda.

Kufuatia hayo, Bw Gisesa alirudi tena kortini na kupata maagizo hayo.

“Kwa sababu ya uzito wa suala lililotajwa hapa, kesi hii itatajwa Machi 12, 2024, na washtakiwa wote wafike kortini,” agizo hilo la mahakama lilisema.

Mji wa Keroka ulianza kuzozaniwa pindi ugatuzi ulivyoanza, lakini magavana waanzilishi–James Ongwae (Kisii) na marehemu John Nyagarama (Nyamira)–walielewana kiustarabu kugawanya mji huo jinsi barabara ya lami inavyougawa mji huo.