Arati, Osoro, Ng’eno na Sonko kuzimwa kuwania viti vya kisiasa

Arati, Osoro, Ng’eno na Sonko kuzimwa kuwania viti vya kisiasa

Na CHARLES WASONGA

WANASIASA na watu ambao majina yao yatawekwa katika orodha ya aibu ya Tume ya Uwiano na Utangamano ya Kitaifa (NCIC) kwa tuhuma za kuchochea chuki, watazimwa kuwania viti katika chaguzi au kushikilia nyadhifa za umma.

Jumatano, tume hiyo ilitangaza kuwa wabunge Simba Arati (Dagoretti Kaskazini), Silvanus Osoro (Mugirango Kusini), Johanna Ng’eno (Emurua Dikirr) na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko ndio wa kwanza majina yao kuwekwa kwenye orodha ya aibu kwa kuhusishwa na uovu huo.

Mwenyekiti wa NCIC, Samuel Kobia aliwaonya wanasiasa hao kwamba endapo wataendelea kuchochea chuki na fujo, majina yao yatawekwa kwa mara ya pili katika orodha hiyo na kutapendekezwa wazimwe kushikilia nyadhifa zozote za umma.

Bw Kobia alisema tume hiyo imeamua kufuata mbinu hiyo kama njia ya kukomesha tabia ya wanasiasa kutoa matamshi ya chuki wakati huu ambapo taifa linajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022 na kura ya BBI.

“Wale ambao tumewahoji na wakasikia kuwa majina yao yatawekwa katika orodha ya aibu wameonekana kuogopa. Hii ina maana kuwa mbinu hii itazaa matunda haswa wakati huu tunapoelekea katika uchaguzi mkuu ujao,” Dkt Kobia akaeleza.

Mwenyekiti huyo alilaani kisa cha juzi ambapo Bw Arati na Bw Osoro walipigana katika mazishi ya babake Naibu Gavana wa Kisii, Joash Maangi.

Dkt Kobia pia alivitaka vyama vya kisiasa kuwachukulia hatua za kinidhamu wanachama wao ambao hukiuka kanuni zake kwa kutoa matamshi ya chuki au kukiuka hitaji la Sura ya Sita la Katiba kuhusu maadili na uongozi bora.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Tukumbuke amani ni deni tutajilipia sisi...

Wanaonipuuza urais 2022 watashangaa – Joho