Makala

Ardhi: Wanakijiji wa Sofia Bona hatarini kufurushwa na NTSA

January 17th, 2024 3 min read

NA LUCY MKANYIKA

WAKAZI wa kijiji cha Sofia Bona, katika eneo la Voi, Kaunti ya Taita Taveta wanaishi kwa hofu ya kufurushwa kutoka kwa makazi yao baada ya Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA) kudai kumiliki ardhi hiyo.

Zaidi ya wakazi 100 ambao wanadai kuishi kwenye kipande hicho cha ardhi cha ekari sita tangu miaka ya sitini (1960s), sasa wana wasiwasi kuwa huenda nyumba zao zikabomolewa na serikali huku mzozo kuhusu umiliki wa eneo hilo ukizidi kutokota.

NTSA tayari imeweka mpaka kuashiria kuwa eneo hilo ni lao.

Wakiongea na Taifa Leo, wakazi hao walikana kuwa ardhi hiyo ni ya serikali na kusema kuwa wameishi hapo hata kabla ya nchi kupata uhuru.

Kwenye kipande hicho cha ardhi kuna nyumba, maduka, na makanisa na sasa wenyeji wanailaumu mamlaka hiyo kwa kukusudia “kunyakua ardhi yao ambayo wanadai waliirithi kutoka kwa mababu zao”.

Mmoja wa wakazi hao, Bi Erestinah Gadi,75, alisema kuwa ameishi hapo tangu Machi 1966 alipoolewa kwa mumewe na kujiunga na familia yake.

Bi Erestinah Gadi akiingia kwa nyumba yake katika kijiji cha Sofia Bona Phase Two kilichoko Voi katika Kaunti ya Taita Taveta. Mama huyo wa umri wa miaka 75 asema ameishi hapo kwa miaka 58 baada ya kuoleka mwaka 1966. NTSA imewataka wakazi kwenye kipande hicho cha ardhi kuondoka. PICHA | LUCY MKANYIKA

Bi Gadi alisema yeye na familia yake wameishi hapo kwa zaidi ya miaka 58 na anashangaa kusikia madai kuwa ardhi hiyo ni mali ya serikali.

“Nilipoolewa na mume wangu nilipata familia yake hapa wakiwemo wazazi wake na ndugu zake. Wote waliaga dunia tukawazika hapa,” akasema Bi Gadi.

Alisema hajui makao mengine kwani wameishi hapo kwa miaka na mumewe na watoto wake.

“Mume wangu alifariki miaka kumi iliyopita na hakuna siku nilisikia akisema hii shamba si yetu. Haya mambo ni mageni kwetu,” akasema.

Alisema licha ya kuona maafisa wa ardhi, wale wa NTSA na maafisa wa polisi wakiweka mpaka, hakuna habari yeyote wamepewa kuhusu umiliki wa ardhi hiyo na nani anayeidai .

“Hatujui tuende wapi. Tunaogopa watarudi na kutubomolea nyumba zetu. Mpaka leo, serikali haijatufikia kutuambia hii sio mali yetu. Katika umri wangu huu nitaenda wapi? Watoto na wajukuu wangu wataenda wapi? Tunahitaji maelezo kwa sababu hakuna mtu aliyetupa habari yoyote,” alisema Bi Gadi.

Anataka serikali badala yake kutafuta ardhi mbadala kwa mradi wao na kutoa hati za umiliki wa ardhi kwa familia zinazoishi kwenye ardhi hiyo.

Alisema juhudi zao za awali za kupimiwa ardhi hiyo hazikufaulu kwani eneo hilo lilirukwa na maafisa wa ardhi wakati wa zoezi hilo miaka kadhaa iliyopita.

“Tulipouliza, walituambia kwamba majina yetu yalikuwa yamenakiliwa tayari. Hatujui kilichotokea baadaye,” alisema.

Mkazi mwingine, Bw Yusuf Rajab alisema juhudi zao za kupata majibu kutoka kwa mamlaka ya NTSA hazikufua kwani maafisa waliokuwa wakisimamia zoezi la upimaji hawakujibu maswali yao.

Mojawapo ya nyumba katika kijiji cha Sofia Bona Phase Two kilichoko Voi katika Kaunti ya Taita Taveta. NTSA imewataka wakazi kwenye kipande hicho cha ardhi kuondoka. PICHA | LUCY MKANYIKA

Haya yanajiri takriban wiki mbili baada ya wakaazi 3,500 wa eneo la Msambweni kubomolewa makazi yao na kampuni binafsi, Sparkle Properties Limited, ambayo ilidai kuwa na amri ya mahakama na mmiliki halisi wa ardhi hiyo.

Aidha, NTSA, imedai kuwa eneo hilo lilitengwa kwa mamlaka hiyo kwa ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa magari tangu 1992.

Mamlaka hiyo ilisema iliwajulisha wakazi kuhusu nia yake ya kuchukua umiliki wa ardhi hiyo na kuwapa muda wa kuondoka eneo hilo ili kuwezesha ujenzi wa kituo hicho.

Afisa anayesimamia huduma za NTSA katika kaunti hiyo Zack Njuguna alisema eneo hilo limekuwa ardhi ya serikali tangu miaka ya 60 na wale waliojenga kwenye ardhi hiyo ni wavamizi.

Bw Njuguna aliambia Taifa Leo kwamba wanapanga kujenga kituo hicho kwa fedha kutoka Benki ya Dunia (WB). Kituo hicho kinakusudiwa kuboresha huduma za ukaguzi wa magari zinazotolewa katika eneo hilo.

“Tuko mbioni ili kupata hati ya ardhi hiyo na punde tu tutakapoipata tutaanza ujenzi wa kituo hicho. Tukichelewa mfadhili anaweza kuondoka kabla ya kutekeleza mradi huo,” alisema Bw Njuguna.

Alisema wamefanya mikutano na wakazi na viongozi wa eneo hilo kuwaelimisha wakazi kuhusu haja ya wao kuondoka katika eneo hilo.

“Tunakabiliwa na upinzani haswa kutoka kwa viongozi wa kisiasa ambao baadhi yao wanawaambia wale wanaokaa kwenye ardhi hiyo wasiondoke. Hata hivyo, tunaongea nao kwani ardhi hiyo ni yetu,” akasema.

Swala la migogoro ya ardhi limekuwa donda sugu katika eneo hilo.

Wenyeji wengi wanaishi kwa hofu bila kujua hatma yao kwa sababu ya ukosefu wa hati miliki za ardhi wanazoishi.

 

Boma mojawapo katika kijiji cha Sofia Bona Phase Two kilichoko Voi katika Kaunti ya Taita Taveta. NTSA imewataka wakazi kwenye kipande hicho cha ardhi kuondoka. PICHA | LUCY MKANYIKA