Habari za Kaunti

Ardhi za Turkana kufanyiwa usoroveya na wakazi kupewa hatimiliki

June 16th, 2024 1 min read

Na SAMMY LUTTA

ARDHI za kijamii katika maeneo kadhaa kaunti ya Turkana sasa zitafanyiwa usoroveya ili wakazi wapewe hatimiliki zitakazowawezesha kulipwa fidia zinapotwaliwa na serikali kwa shughuli za maendeleo.

Mkurugenzi wa Idara ya Usoroveya katika kaunti hiyo Joseph Egiron amesema kuwa shughuli hiyo imeanza katika maeneo ya Lokichar, kaunti ndogo ya Turkana Kusini na Nakukulas katika kaunti ndogo ya Turkana Mashariki.

“Kufikia mwishoni mwa Julai mwaka huu wakazi katika maeneo haya wataanza kupokea hatimiliki kwa ardhi zao,” akasema.

Bw Egiron alisema kundi la maafisa wa kiufundi kutoka Idara ya Ardhi, Nyumba, Ujenzi na Usimamizi wa Miji na wenzao kutoka Wizara ya Ardhi katika serikali ya kitaifa wanasaidiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Kilimo na Chakula (FAO) kuendesha shughuli hiyo ya usoroveya.

“Shughuli hii itawezesha utoaji hatimiliki tofauti kwa asasi za umma kama vile shule na vituo vya afya,” akaongeza.

Shughuli hiyo ya usoroveya na utoaji hatimiliki ni sehemu ya mpango wa Gavana wa Turkana Jeremiah Lomorukai kuhakikisha kuwa wakazi wanarasimisha umiliki wa ardhi zao.

Kampuni ya Tullow Oil ilipogundua utajiri wa mafuta katika kaunti ndogo ya Turkana Kusini 2012, ardhi za kijamii zilitwaliwa kwa ujenzi wa barabara, uchimbaji wa visima vya mafuta na ujenzi wa miradi mingine ya maendeleo.

Lakini wakazi wa eneo hilo walikosa kulipwa fidia kwa ardhi zao za kijamii kwa sababu ya kukosa hatimiliki.