Argentina na Paraguay waambulia sare tasa katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022

Argentina na Paraguay waambulia sare tasa katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022

Na MASHIRIKA

ARGENTINA walishindwa kupenya ngome ya Paraguay waliowalazimishia sare tasa katika mechi ya Alhamisi usiku kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia mnamo 2022 nchini Qatar.

Wageni Argentina walikosa huduma za fowadi matata wa Inter Milan, Lautaro Martinez katika mchuano huo uliowakutanisha mjini Asuncion. Hali hiyo iliwawia vigumu kuelekeza makombora mazito langoni mwa Paraguay.

Joaquin Correa alikosa fursa ya kuwaweka Argentina kifua mbele huku Lionel Messi akishuhudia mikwaju yake ya frikiki ikikosa kuzaa matunda aliyotarajia.

Kwa upande wake, Paraguay nusura wafunge bao kupitia Carlos Gonzalez dakika mbili kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo.

Mwishoni mwa mechi, mashabiki walivamia uwanja kwa nia ya kupiga picha na Messi.

Brazil, ambao wameshinda mechi zote tisa za kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia, sasa wanaselelea kileleni mwa orodha ya wawakilishi wa soka kutoka Amerika Kusini kwa alama 27. Argentina wanashikilia nafasi ya pili kwa pointi 19, tatu kuliko Ecuador na Uruguay wanaofunga orodha ya nne-bora.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Raphinha awabeba Brazil dhidi ya Venezuela katika mechi ya...

Afueni wakazi wa Carwash-Zimmerman wakiimarishiwa barabara