Argentina waangusha Paraguay huku Chile wakitoka nguvu sawa na Uruguay kwenye Copa America

Argentina waangusha Paraguay huku Chile wakitoka nguvu sawa na Uruguay kwenye Copa America

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

ARGENTINA walikalia vizuri kileleni mwa Kundi A kwenye kampeni za Copa America zinazoendelea nchini Brazil baada ya kupepeta Paraguay 1-0 mnamo Jumatatu usiku.

Bao la pekee katika mechi hiyo lilifumwa wavuni na nyota Alejandro Dario Gomez katika dakika ya 10. Chini ya kocha Lionel Scaloni, Argentina kwa sasa wanaselelea kileleni mwa Kundi A kwa alama saba, mbili zaidi kuliko nambari mbili Chile walioambulia sare ya 1-1 dhidi ya Uruguay.

Chile waliwekwa kifua mbele na Eduardo Vargas katika dakika ya 26 kabla ya Arturo Vidal kujifunga na kusawazishia Uruguay ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne kwa alama moja, nyuma ya Paraguay ambao wamejizolea pointi tatu kutokana na mechi mbili zilizopita.

Chini ya mkufunzi Oscar Tabarez, Uruguay inayojivunia maarifa ya vigogo Edinson Cavani na Luis Suarez, walizidiwa maarifa na Argentina kwa 1-0 mnamo Juni 18 jijini Brasillia.Kwa upande wao, Chile walikuwa wamejizolea pointi nne kutokana na mechi mbili zilizopita baada ya kuwalazimishia Argentina sare ya 1-1 mnamo Juni 15 kabla ya kupepeta Bolivia 1-0 siku nne baadaye.

Mechi dhidi ya Argentina ilikuwa ya nne mfululizo kwa Uruguay kukamilisha bila ya kusajili ushindi tangu Novemba 13, 2020 walipowapiga Colombia 3-0 kwenye mojawapo ya mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Waliambulia sare tasa dhidi ya Paraguay na Venezuela mnamo Juni 4 na Juni 9 baada ya kutandikwa 2-0 na Brazil mnamo Novemba 18, 2020. Argentina waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Chile na kuwakung’uta Uruguay 1-0 katika mechi mbili za kwanza kundini. Paraguay walifungua kampeni za Kundi A kwa kucharaza Bolivia 3-1.

Jumla ya vikosi vinne miongoni mwa vitano vinavyounga Kundi A na na vinne vingine kutoka Kundi B linaloongozwa sasa na wenyeji Brazil, vitafuzu kwa hatua ya nane-bora.Mbali na Argentina na Chile, vikosi vingine vinavyopigiwa upatu wa kusonga mbele kutoka Kundi A ni Paraguay na Uruguay.

Bolivia hawana alama yoyote baada ya kupoteza mechi mbili zilizopita. Walipigwa 3-1 na Paraguay mnamo Juni 15 kabla ya kucharazwa 1-0 na Chile siku tatu baadaye. Huku Paraguay wakijivunia kutawazwa mabingwa wa Copa America mnamo 1953 na 1979, Bolivia wamewahi kusonga mbele kutoka hatua ya makundi ya kipute hicho mara moja pekee, hiyo ikiwa mnamo 2015 ambapo walipigwa 3-1 na Peru kwenye robo-fainali.

Argentina walishuka dimbani wakijivunia rekodi ya kutoshindwa tangu 2019. Hata hivyo, wanafainali hao wa Kombe la Dunia mnamo 2014 na Copa America mnamo 2019, hawajawahi kutia kapuni taji la Copa America kwa takriban miaka 30 iliyopita. Mara yao ya mwisho kutawazwa mabingwa wa Copa America ni 1993.

Ingawa hivyo, wamejisuka upya na wanajivunia mwamko mpya chini ya Scaloni tangu wabanduliwe mapema na Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi. Mikoba yao ilikuwa ikidhibitiwa na kocha Jorge Sampaoli wakati huo.

Chile wana kiu ya kutia kibindoni taji la tatu la Copa America baada ya kutawazwa mabingwa mnamo 2015 na 2016. Licha ya miaka mitano kupita tangu wanyanyue taji la mwisho la Copa America, kikosi cha kwanza cha Chile hakijabadilika pakubwa huku Alexis Sanchez wa Inter Milan (Italia) na Eduardo Vargas wa Atletico Mineiro (Brazil) wakisalia tegemeo kubwa katika safu ya mbele.

  • Tags

You can share this post!

Ndoa ya Jubilee na ODM yapigwa mawe