Arror, Kimwarer: Mashahidi sasa walia kutishwa

Arror, Kimwarer: Mashahidi sasa walia kutishwa

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) jana alifichua mashahidi wakuu katika kesi ya kashfa ya mabwawa ya Arror na Kimwarer ya Sh63 bilioni inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Bw Henry Rotich kwamba wametishwa na hawataki kufika kortini kutoa ushahidi.

Kupitia viongozi wa mashtaka Taib Ali Taib, Alexander Muteti na Vincent Monda , DPP alimweleza hakimu mkuu Lawrence Mugambi , kuwa tayari uchunguzi umeanza kufanywa na afisi ya mkurugenzi wa jinai (DCI) kuwatambua wanaotoa vitisho dhidi ya mashahidi kwa lengo la kuwachukulia hatua za kisheria.

Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Bw Henry Rotich akiwa kortini Alhamisi, Septemba 22, 2022. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Mmoja wa mashahidi hao Gideon Rotich, alifika kortini Alhamisi na kukataa kutoa ushahidi akisema ananaogopa na kwamba hakuwa ameelezwa awali atafika kortini kutoa ushahidi katika kesi ya kashfa hiyo.

Bw Rotich , anayefanya kazi katika mamlaka ya mazingira (NEMA) aliomba muda ajifahamishe kuhusu ushahidi atakaotoa kortini.

“Nilipigiwa simu na afisa kutoka DCI mnamo Septemba 19, 2022 na kuelezwa nifike kortini bila kukosa. Leo nimekutana na viongozi wa mashtaka kwenye veranda na kunieleza nijiandae kutoa ushahidi kortini,” Bw Rotich alimweleza hakimu.

Hata hivyo, aliomba muda ajiandae kutoa ushahidi akisema ameingiwa na woga.

“Sijajiandaa kimawazo kusimama kizimbani kutoa ushahidi. Hii ndiyo mara yangu ya kwanza kufika kortini,” akasema Bw Rotich.

Katika mawasilisho yao Mabw Taib, Muteti na Monda walisema wamepokea ripoti kwamba mashahidi wamekuwa wakitishwa na washtakiwa.

“Mashahidi wamepokea vitisho na sasa hawataki kufika kortini kusimulia kilichojiri,” Bw Taib alifichua.

Alisema hataki makabiliano na mawakili wa washtakiwa na kugeuza mahakama kuwa “ulingo wa soko lisilo na utaratibu na mwelekeo. Tutawasilisha ombi kamili kujadiliana suala hili”.

Bw Muteti alimweleza hakimu kuwa amethibitishiwa na maafisa wa DCI kwamba mashahidi wamepokea vitisho na wanahofia maisha yao.

Mahakama ilielezwa kuwa tayari ripoti hizi zinachunguzwa na maafisa wa DCI.

Bw Taib alisema ombi maalum litawasilishwa kuhusu suala hilo ili korti itoe maagizo kamili.

Bw Mugambi alimhoji Bw Rotich (shahidi) kwa muda mrefu ndipo abaini ukweli kutokana na mfanyakazi huyo wa Nema kuogopa.

“Ninaipa afisi ya DPP muda ifanye mashauri na mashahidi kisha iwaandae kabla ya kufika kortini kutoa ushahidi.

“Sitaki kuwashurutisha mashahidi kufika kortini. Wanatakiwa kuja kwa hiari wakijua kinachowaleta kortini na kutoa ushahidi kusaidia korti kutenda haki,” alisema Bw Mugambi.

Awali wakili Kioko Kilukumi alikuwa amepinga Bw Roticha kutoa ushahidi akidai alikuwa ameorodheshwa kuwa nambari 28 na wala sio shahidi wa pili.

Bw Kilukumi pia alikuwa amesema DPP aliwapa taarifa ya ushahidi wa Rotich Jumatano usiku.

Kesi iliahirishwa hadi Novemba 18, 2022.

  • Tags

You can share this post!

Nassir ateua aliyekuwa katibu wa KMPDU kuongoza kamati ya...

Macho kwa Neymar timu ya Brazil ikiendea Ghana kirafiki leo

T L