Michezo

Arsenal dimbani dhidi ya Spurs ikilenga kuzuia pancha

April 28th, 2024 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

HOFU inayoandamana na taharuki imetanda kwa mashabiki wa klabu ya Arsenal ambayo kwa misimu kadhaa sasa, imekuwa ikianza vizuri lakini ikiishiwa pumzi pale ukingoni mwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Leo Jumapili, Arsenal itavaana na mashemeji wake wa London Kaskazini ambao ni Tottenham Hotspur, hisia za sare, kupoteza au kupata alama zote tatu, zimetawala fikra za mashabiki.

“Hii ni siku ya debi na kama mjuavyo, debi huwa kama vita vya ukombozi wa kujipa uhuru. Ni mtanange wa jasho, machozi na hata damu. Ni mechi ya kadi tele hata zile nyekundu,” akasema Seneta Maalum Karen Nyamu akihojiwa na Taifa Spoti kuhusu mechi hiyo itakayoanza saa kumi jioni.

Seneta huyo ambaye ni shabiki sugu wa Arsenal alisema wako roho juu kwamba The Gunners itawika.

“Lakini udadisi wangu ni kwamba mechi ni ngumu na uhalisia wangu ni kwamba nitakubali matokeo,” akasema.

Ingawa hivyo, alisema imani yake haiko kwa sare au kushindwa kwa kuwa pale tuko ni “Mungu na serikali saidia kwa kuwa mechi nne zilizosalia ni lazima tuzishinde huku tukiomba Man City iliyo nyuma yetu angalau katika mechi tano iliyosalia nazo ilimwe angalau kwa moja au itoke sare moja tu”.

Bi Nyamu alisema takwimu haziko sawa vile kwa Arsenal kwa kuwa zinaashiria hali ya eti eti.

Arsenal katika historia ya ushindani ambao hadi sasa ni mara 208, Spurs imeshinda mara 86 huku Arsenal ikishinda mara 67 na kutoka sare mara 55.

Licha ya kufahamika kama Wanabunduki, katika awamu ya lala salama ya vita vya ubingwa wa EPL, huwa wanafahamika kwa kuwa wabutu wa kulenga visivyo na kuishia kujihujumu katika mechi muhimu za mwisho.

Mtanange huu wa Jumapili utakuwa na umuhimu mkuu kwa timu zote mbili kwa kuwa Arsenal ikilenga taji la EPL ambalo limewaponyoka kwa miaka zaidi ya 20 hadi sasa, Spurs wanalenga kumaliza ndani ya nne bora ili kushiriki dimba la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Spurs kwa sasa iko katika nafasi ya tano ikiwa na pointi 60 huku Aston Villa ikiwa ya nne kwa pointi 67 lakini Spurs ikiwa na mechi tatu kibindoni ambapo ikizishinda, itapaa hadi pointi 69.

Spurs inafaa kuwachinjia mbuzi wachezaji wa Chelsea ambao Jumamosi waliishika Aston Villa na kulazimisha sare ya 2-2.

Kama Villa wangeibuka na ushindi kama walivyozoea katika siku nyingi za msimu huu, ukiwemo ule wa dhidi ya Arsenal, wangejipata kwa pointi 69 hivyo basi kufanya hesabu ya Spurs kuwa ngumu.

Hesabu ya Arsenal inaingia katika taswira ya msimu jana ambapo wengi walikuwa tayari kuweka beti ya uhai wao kwa timu hii kuibuka bingwa wa EPL.

Lakini sare dhidi ya Liverpool, West Ham United na Southampton (iliyokuwa ikielekea kushushwa daraja) pamoja na vichapo mikononi mwa Nottingham Forest, Brighton na Manchester City vilisukuma Arsenal hadi nafasi ya pili kwa pointi 84 dhidi ya washindi–Man City–waliozoa pointi 89.

Kwa sasa, iwapo kila timu mojawapo ya hizi mbili kubwa itashinda mechi zake zilizosalia, Man City itaibuka bingwa kwa pointi 91, Arsenal ya pili kwa pointi 89 nayo Liverpool iwe ya tatu kwa pointi 84 huku Tottenham ikiwa ya nne kwa pointi 78.

Shida ni kwamba, Tottenham iko na mechi leo Jumapili na Arsenal, iko na kibarua na Man City na bado na Liverpool hivyo basi kumaanisha kunao watapoteza pointi, hali ambayo inaifanya ligi hii kuwa ya kukaza tu.

Ilivyo kwa sasa ni kwamba, Tottenham Hotspur iko na ufunguo wa ni nani ataibuka bingwa wa ligi hii ya EPL msimu huu.