Michezo

Arsenal ilivyoanguka toka kileleni hadi shimo la aibu

August 4th, 2020 6 min read

Na CHRIS ADUNGO

Ilikuwa Jumatano, Mei tarehe 17 mwaka wa 2006. Mashabiki walishiba matumaini kuwa hatimaye kikosi chao pendwa kingeingia katika kilinge cha ‘timu kubwa’ za barani Ulaya kwa kunyakua taji maarufu linalotamaniwa na kila timu ya Uropa.

Nyoyo ziliwadunda dududu! Wengi si tu kwa hofu ya kutojua lipi lingetokea bali pia kwa shauku ya kupepeta majabali wa kandanda duniani, Barcelona kwenye safari ya kujizulia fahari ya kihistoria katika uwepo wao wa zaidi ya karne moja.

Kwa upande wa Arsenal, walikuwepo wachawi wa soka kama vile Thierry Henry, Alexandre Hleb, Frieddie Ljungberg, Cesc Fabregas, Kolou Toure, na kipa Jens Lehmann chini ya ualimu wa Prof Arsene Wenger huku wauaji Ronaldinho Gaucho, Samuel Eto’o, Carles Puyol na mnyakaji Victor Valdes chini ya mkufunzi Frank Rijkaard wakifanyia Barcelona vitu vyao.

Arsenal, wakiwa wamevalia jezi zao za njano, kwa hisani ya Henry, walianza kubabaisha ‘zambarau-nyeusi’ Barcelona, hali iliyopekecha matumaini yao kuwa, kwa mara ya kwanza, timu yao ilielekea kutwaa taji la UEFA Champions League.

Jambo ambalo hawakulijua ni kuwa dakika 18 pekee baada ya mechi kung’oa nanga, kipa Lehmann angeoneshwa kadi nyekundu kwa madai kuwa alimchezea Eto’o ngware nje kidogo ya kisanduku. Kadi hiyo kwa hakika, kwa mujibu wa wadadisi wa kandanda, haikufaa.

Ila liandikwalo ndilo liwalo. Hata hivyo, la ajabu lilikuwa kuwa licha ya The Gunners kusalia na wanasoka 10 pekee, ndio walioanza kufunga bao kwa mizungu ya Sol Campbell.

Bao hilo lilikombolewa dakika ya 76 na Eto’o. Dakika nne baadaye Juliano Belleti alivunja kabisa matumaini ya mashabiki wa Arsenal kwa kumfunga Manuel Alumnia bao chungu. Gozi likaisha 2-1.Arsenal ikasalia miongoni mwa timu chache kubwa za Uingereza zisizowahi kutwaa taji hili.

Hicho kwa hakika ndicho kilichokuwa kilele cha soka safi ya Arsenal, maadamu kuanzia hapo klabu hii ya Kaskazini mwa London, Uingereza haijawahi kushinda taji la maana isipokuwa Kombe la FA ambalo imelishinda mara 14 -ikiwa ni rekodi kwani hakuna timu nyingine iliyolishinda kuzidi hapo.

Miaka miwili kabla ya fainali hiyo ya UEFA iliyochezewa Ufaransa, Arsenal ilikuwa imeshinda taji lake la 13 la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), taji ambalo ndilo la mwisho timu hii kuwahi kunyakua.

Hadi sasa Arsenal imesalia kuwa ombwe au kaka tupu la yai maadamu haitambi tena, si ligini, si katika Europa League wala Uefa Champions League.

Hii ni licha ya kuweka mikakati kabambe ya kuifufua; Wenger hatimaye alionyeshwa paa, akaja Unai Emery aliyebambanya kidogo na kumpisha kijana Mikel Arteta aliye usukani hadi sasa.

Hii ndiyo maana mwandishi wetu amezama na kuibuka na makala bomba kuhusu kuinuka ajabu na kisha kuporomoka hadi ikabaki kigaye kitupu.

1996 – 2018

Arsenal walikamilisha kampeni za EPL msimu huu katika nafasi ya nane kwa alama 56. Hii ndiyo nambari mbovu zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kukamata katika historia ya EPL tangu 1995.

Matatizo mengi ya ndani na nje ya uwanja yamekuwa kiini cha kushuka kwa makali ya Arsenal ambao kwa sasa wamekuwa wakisajili matokeo ya kutotabirika kabisa katika takriban kila mechi ligini.

Chini ya Wenger aliyewahudumia kwa miaka 22 kati ya 1996 na 2018, Arsenal walinyanyua ubingwa wa EPL mara tatu (1997-98, 2001-02, 2003-04) na kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mara moja (2005-06).

Haya ndiyo mafanikio makubwa zaidi kwa Arsenal kwenye EPL katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Tangu wakati huo, Arsenal wamekuwa na ukame wa taji la EPL huku panda-shuka zao zikihusishwa na mbinu mbovu za ukufunzi; kutokuwa wepesi wa kujifunza kutokana na makosa ya awali; na utepetevu wa wachezaji ambao wamesalia wanyonge dhidi ya wapinzani wakuu ligini.

Ubahili wa Arsenal; sera duni za usajili na usimamizi mbaya wa mikataba ambao umewafanya kuagana ghafla na wanasoka tegemeo ni miongoni mwa sababu nyinginezo za kudorora kwa kikosi hicho.

Robin van Persie, Gael Clichy, Bacary Sagna, Alexis Sanchez, Alex Oxlade-Chamberlain, Fabregas na Aaron Ramsey ni kati ya wanasoka wa haiba waliowahi kuondoka Emirates baada ya Arsenal kuwashawishi warefushe kandarasi zao kwa wakati ufaao.

Ikumbukwe kuwa hakuna mwanasoka yeyote matata zaidi wa enzi hii ambaye hajawahi kuhusishwa na uwezekano wa kutua Arsenal baada ya upekee wao kutambuliwa na Wenger aliyezingirwa na maskauti hodari wa kusaka vipaji.

Kylian Mbappe, Raheem Sterling, Luis Suarez, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wamewahi kuhusishwa na Arsenal.

Baada ya kukatiza uhusiano na Wenger mwishoni mwa msimu wa 2017-18 uliowashuhudia wakitupwa hadi nafasi ya sita, Arsenal wameajiri makocha wawili – UEmery na Arteta kwa matumaini ya kurejea ndani ya mduara wa nne-bora kwenye jedwali la EPL.

Katika jaribio la kwanza la Emery, Arsenal waliambulia nafasi ya tano mnamo 2018-19 na kocha huyo akatimuliwa Novemba 2019.

Hadi 2017-18, Arsenal walikuwa wamekamilisha kampeni za EPL nje ya orodha ya nne-bora mara saba chini ya Wenger (1998-99, 2005-06, 2008-09, 2011-12, 2012-13, 2014-15).

Masaibu ya Arsenal katika EPL yalianza 2004-05 baada ya kushindwa kuhifadhi ubingwa walionyanyua bila kupoteza hata mechi moja katika msimu wa 2003-04 walipopewa jina The Invincibles yaani Wasioshindwa.

Ni mnamo 2005 ambapo waliagana rasmi na kiungo tegemeo mzawa wa Ufaransa, Patrick Vieira aliyeyoyomea Juventus.

Thierry Henry

2005-06: Huu ulikuwa msimu wa mwisho wa Arsenal uwanjani Highbury na ndio uliokuwa mbaya zaidi tangu kuajiriwa kwa Wenger. Arsenal walipoteza mechi 11 na wakamsajili kiungo Abou Diaby na fowadi Emmanuel Adebayor.

2006-07: Arsenal walifunga idadi chache zaidi ya mabao (68) chini ya Wenger.

Magoli ya siku ya mwisho ya msimu kutoka kwa Diaby, Adebayor na Thierry Henry yaliwaepushia aibu ya kutupwa nje ya nne-bora.

Ukufunzi wa Wenger ulianza kutiliwa shaka baada ya kubanduliwa nje ya UEFA kwenye hatua ya 16-bora.

2007-08: Arsenal walijinyanyua na kukamata nafasi ya tatu kwa alama 83. Hata hivyo, walipokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Man-United siku ya mwisho ya msimu na kuagana na Gilberto Silva na Mathieu Flamini. Mapengo ya wawili hao hayakuzibwa.

2008-09: Arsenal waliambulia nafasi ya nne kwenye jedwali la EPL huku pengo la pointi 18 likitamalaki kati yao na mabingwa Man-United. Umri wastani wa wanasoka waliowategemea hadi kutinga nusu-fainali ya UEFA ulikuwa kati ya miaka 23 na 24.

Wenger alishauriwa kusajili kiungo kizibo cha Vieira lakini akakataa na kuzidisha imani yake kwa chipukizi.

2009-10: Arsenal walizinadi huduma za Adebayor na Wenger akakataa kununua mshambuliaji mpya wala kiungo mkabaji wa haiba.

Walitinga robo-fainali ya UEFA na kukamilisha EPL katika nafasi ya tatu kwa alama 75, pointi 11 nyuma ya mabingwa Chelsea.

Mashabiki walianza sasa kushinikiza usimamizi kumtimua Wenger kwa kubeba mabango ya maandishi ‘Wenger Out’ mwishoni mwa takriban kila mechi uwanjani.

2010-11: Kipa chaguo la kwanza, Wojciech Szczesny alipata jeraha baya lililomweka mkekani kwa kipindi kirefu.

Nafasi yake ilitwaliwa na Manuel Almunia aliyeshindwa kung’aa. Kigogo Jens Lehmann aliyestaafu alirejea ugani Emirates kuwadakia Arsenal baada ya walinda-lango Almunia, Lukasz Fabianski na Vito Mannone pia kujeruhiwa.

Newcastle United waliweka historia ya kutoka chini kwa 4-0 na kulazimishia Arsenal sare ya 4-4. Arsenal walibanduliwa na Birmingham City kwenye League Cup, Man-United wakawadengua kwenye Kombe la FA na hatua ya 16-bora ya UEFA.

2011-12: Kiungo mbunifu Cesc Fabregas alibanduka ugani Emirates na kuyoyomea Barcelona. Chombo cha Arsenal kilisalia ovyo na kikaanza kuvuja. Arsenal walipondwa 8-2 na Man-United ugani Old Trafford.

Wenger aligutuka na kusajili wanasoka haraka; Yossi Benayoun, Mikel Arteta, Per Mertesacker, Andre Santos na Park Chu-Young ingawa ujio wao ulikosa kuziba nyufa za kikosi chake kilichopepetwa 4-0 na AC Milan kwenye UEFA.

Arsenal walimaliza EPL katika nafasi ya tatu kwa alama 70, pointi 19 nyuma ya wafalme Man-City.

2012-13: Arsenal waliagana na mfumaji mahiri Robin van Persie ambaye aliingia katika sajili rasmi ya Man-United alikotwaa taji la EPL na kuibuka mfungaji bora wa msimu.

Wenger alimwachilia pia kiungo matata Alex Song kujiunga na Barcelona huku Arsenal wakijinasia huduma za Lukas Podolski, Olivier Giroud, Santi Cazorla na Nacho Monreal.

Licha ya kujisuka upya, Arsenal walishindwa kupata kizibo kamili cha Van Persie na Song. Waliambulia nafasi ya nne kwa alama 73, pointi 15 nyuma ya mabingwa Man-United.

2013-14: Ujio wa Mesut Ozil kutoka Real Madrid uliwasisimua mashabiki wa Arsenal. Hata hivyo, Wenger alisalia yule yule na akakataa kuimarisha uthabiti wa safu ya ulinzi na idara ya uvamizi.

Mathiu Flamini alirejea upya ugani Emirates ila hakung’aa sana kama alivyofanya 2008. Arsenal waligeuka mteremko kwa miamba wa soka ya EPL.

Walipepetwa 5-1 na Liverpool, wakatandikwa 6-3 na Man-City na Chelsea ikawakomoa 6-0 katika mechi ya 1,000 ya Wenger katika taaluma kazi ya ya ukocha.

Arsenal walitwaa Kombe la FA, wakabanduliwa kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA na wakakamata nafasi ya nne ligini kwa alama 79, saba nyuma ya mabingwa Man-City.

2014-15: Arsenal walisajili nyota Alexis Sanchez, kipa David Ospina na beki Calum Chambers. Beki Bacary Sagna aliondoka na nafasi yake kutwaliwa na Mathieu Debuchy.

Licha ya Aaron Ramsey na Jack Wilshere kutambisha safu ya kati, Arsenal walikosa fowadi mahiri wa kushirikiana na Sanchez.

Walimsajili Danny Welbeck kwa pupa kutoka Man-United siku ya mwisho. Ingawa walishinda Kombe la FA, walibanduliwa kwenye UEFA katika hatua ya 16-bora na wakafunga mduara wa tatu-bora ligini kwa alama 75, pointi 12 nyuma ya mabingwa Chelsea.

2015-16: Arsenal walimsajili kipa Petr Cech na kiungo Mohamed Elneny kutoka Chelsea na FC Basel mtawalia. Hata hivyo, udhaifu wao ulisalia kwenye safu ya kati na idara ya ulinzi.

Leicester City walijizolea alama 81 na kutwaa ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 132.

Arsenal waliridhika na nafasi ya pili kwa pointi 71.

2016-17: Baada ya kuacha wanasoka mahiri kama vile mvamizi N’golo Kante aliyejiunga na mabingwa wa mwaka huo, Chelsea, The Gunners walisajili kivoloya, hali iliyochangia chombo chao kiyumba zaidi na wakamaliza msimu nje ya mduara wa nne-bora kwa mara ya kwanza chini ya Wenger aliyeokolewa na ushindi wa Kombe la FA dhidi ya Chelsea.

Tottenham walimaliza EPL mbele ya Arsenal kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22.