Michezo

Arsenal inayomhemea beki Kimmich wa Bayern yaambiwa ‘tuongee baada ya kazi’

April 6th, 2024 1 min read

TETESI ZA MASTAA

NA CECIL ODONGO

MIAMBA wa Ujerumani (Bundesliga), Bayern Munich, wameambia Arsenal watulize boli kwanza hadi mwisho wa msimu huu ili kujadili uwezekano wa kumsajili Joshua Kimmich.

Inaaminika Gunners wamewasiliana na Bayern lakini wakaambiwa hakuna mazungumzo kabla msimu kutamatika.

Gumzo linadai Arsenal wanamuona raia huyo wa Ujerumani kama mchezaji muhimu atakayeimarisha kikosi chao hivyo watazidisha mivizio msimu unapoelekea ukingoni.

Kocha Mikel Arteta anapenda wachezaji wanaoweza kucheza nafasi kadhaa katika safu zao.

Gunners wataingia sokoni kusaka mwanasoka anayeweza kucheza kama beki wa pembeni kulia na pia k safu ya kati kusaidia katika mashambulizi.

Ingawa Kimmich yuko sawa safu ya kati, naibu nahodha huyo wa Bayern amechezeshwa kama beki klabuni na pia timu ya taifa.

***

Nagelsmann naye pia amezewa mate kutwaa mikoba ya Man United

JULIAN Nagelsmann ni kocha wa hivi punde kuhusishwa na Manchester United.

United wanaaminika kumezea mate makocha kadhaa kismati cha Erik ten Hag ugani Old Trafford kikididimia kutokana na matokeo ya kutoridhisha.

Orodha ya makocha ambao wamehusishwa na mikoba ya Red Devils iwapo Ten Hag atatimuliwa inajumuisha Nagelsmann aliyezinoa Bayern Munich na Leipzig zote katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Pia kuna Kieran McKenna wa Ipswich Town katika Ligi Ya Daraja ya Pili Uingereza (Championship), Graham Potter aliyenoa Brighton na Chelsea katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Thomas Tuchel wa Bayern na Roberto De Zerbi wa Brighton.

Ten Hag, ambaye amesalia na msimu mmoja katika kandarasi yake kambini mwa United, inaaminika anaweza kupigwa shoka mwisho wa msimu huu na anakabiliwa na presha kweli kweli.

Mholanzi huyo ameambulia matokeo mabovu mara si haba kinyume na matarajio ya mashabiki na wamiliki wa Red Devils.

Dua ya Ten Hag kupewa muda zaidi Old Trafford ili abadilishe mkondo wa matokeo ilipata pigo baada ya sare ya 1-1 na Brentford mnamo Jumamosi iliyopita.