Michezo

ARSENAL ITAWEZA? Liverpool kukabiliana na Arsenal leo usiku

October 30th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MERSEYSIDE, Uingereza

LIVERPOOL na Arsenal zitakabiliana leo Jumatano usiku kutafuta nafasi ya kufuzu kwa robo-fainali ya Carabao Cup.

Mabingwa wa taji la Klabu Bingwa barani Ulaya, Liverpool ya kocha Jurgen Klopp, wanapewa nafasi kubwa ya kupata ushindi dhidi ya Arsenal.

Wakati huu wanaendelea kufurahia uongozi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa pointi sita mwishoni mwa wiki kwa kuandikisha ushindi wa 2-1 dhidi ya Tottenham Hotspur.

Kwa upande mwingine, Arsenal wanakabiliwa na matatizo mengi baada ya kuagana 2-2 na Crystal Palace katika mechi nyingine ya EPL ambayo waliongoza kwa 2-0 kabla ya wapinzani wao kutoka nyuma na kusawazisha.

Mapema juma hili, klabu hiyo ilikuwa ikifikiria kumpokonya unahodha Granit Xhaka kufuatia kitendo chake cha kuwadharau mashabiki wa klabu hiyo ugani Emirates, huku kocha wao Unai Emery akikabiliwa na hali ngumu kufutaia matokeo duni.

Kutokana na hasira za kocha huyo, lazima meneja huyo apate ushindi katika pambano la leo ugani Anfield, lakini huenda asifanikiwe kutokana na kikosi imara cha Klopp ambaye anatafuta mataji matatu msimu huu.

Huenda Mohamed Salah asianze mechi ya leo baada ya kutolewa uwanjani baada ya kuumia wakicheza na Spurs.

Beki Virgil van Dijk aliumia siku hiyo na huenda akapumzishwa, sawa na Joel Matip ambaye anauguza jeraha la goti.

Vilevile Klopp atakosa huduma za Xherdan Shaqiri na Nathaniel Clyde, lakini kocha huyo anayedhaniwa kutumia mfumo wa 4-3-3, anatarajiwa kuanza na Adrian, Milner, Lovren, Gomez, Robertson, Oxlade-Chamberlain, Henderson, Keita, Lallana, Origi na Mane.

Kwa upande mwingine, Emery anatarajiwa kuifanyia mabadiliko timu yake ili makinda kadhaa wapate fursa ya kuonyesha vipaji vyao hadharani.

Huenda Xhaka akatemwa ili Joe Willock ajaze nafasi hiyo, lakini mashabiki wengi wamemsihi kocha Emery aunde kikosi sawa na kile kilichowakilisha timu hiyo katika mechi za Europa League, akimshirikisha Kieran Tierney kama beki wa upande wa kushoto.

Kadhalika, mashabiki wanatarajia Gabriel Martinelli na Bukayo Saka kuanza kama mabeki wa katikati, baada ya ushirikiano wao kuonekana kuwa mwema.

Kikosi cha Arsenal kinatarajiwa kuwa na Martinez, Bellerin, David Luiz, Kolasinac, Torreira, Willock, Maitland,-Niles, Smith Rowe, Saka na Martinelli.

Liverpool wanajivunia rekodi nzuri ya ushindi 88 na sare 61 dhidi ya Arsenal ambao wameibuka na ushindi mara 78.

Mbali na historia hiyo, Liverpool hawajashindwa katika mechi zao tisa za karibuni dhidi ya vijana hao wa Emery, huku wakijivunia ushindi mara tano, ukiwemo wa 5-1 na 3-1 zilipokutana Desemba 2018 na Agosti 2019.