Michezo

Arsenal kualika Manchester United usiku

January 1st, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

ARSENAL inakabiliwa na kibarua kingine kigumu inapotafuta ushindi wake wa kwanza katika mechi saba kwenye Ligi Kuu katika uwanja wake wa nyumbani wa Emirates itakapofufua uadui na Manchester United, leo Jumatano.

Vijana wa Mikel Arteta wamepata alama mbili kutoka mechi zao sita zilizopita za nyumbani ligini baada ya kutoka 2-2 dhidi ya Crystal Palace (Oktoba 27), Wolves 1-1 (Novemba 2) na Southampton 2-2 (Novemba 23) kabla ya kulimwa na Brighton 2-1 (Desemba 5), Manchester City 3-0 (Desemba 15) na Chelsea 2-1 (Desemba 29).

Mara ya mwisho Arsenal ilivuna ushindi ligini mbele ya mashabiki wake wa nyumbani ilikuwa Oktoba 6 ilipolaza Bournemouth 1-0.

Beki David Luiz, ambaye alifungia Arsenal bao lililozamisha Bournemouth, anatarajiwa kuwa na shughuli nyingi ya kuzuia mashambulizi makali kutoka kwa United ambayo imeonyesha kivumbi timu kubwa kama Manchester City, Tottenham Hotspur, Chelsea na Leicester pamoja na kugawana alama na viongozi Liverpool.

Arsenal itaanza mchuano huu wao wa 232 dhidi ya United alama sita pekee nje ya mduara hatari wa kutemwa kwa hivyo itakuwa na presha ya kufungua mwaka 2020 vyema ili kujiondoa katika maeneo hayo.

Wanabunduki wa Arsenal walipiga United 2-0 kupitia mabao ya Granit Xhaka na Pierre-Emerick Aubameyang wakati timu hizi zilikutana mara ya mwisho uwanjani Emirates mwezi Machi 2019.

Hata hivyo, tangu wakati huo Arsenal imepiga hatua nyingi nyuma nayo United imeamka kwa hivyo vijana wa Ole Gunnar Solskjaer ndio watakaoanza mechi hii ya raundi ya 21 wakijivunia asilimia kubwa ya kuishinda.

Arsenal imeonyesha kuimarika kimchezo tangu iajiri Arteta japo imeambulia alama moja kutoka mechi mbili ameongoza timu hii baada ya kutoka nyuma na kukaba Bournemouth 1-1 mnamo Desemba 26 na kutupa uongozi ikichapwa na Chelsea 2-1 siku nne zilizopita.