Arsenal kumwachilia Willian ayoyomee Inter Miami inayomilikiwa na Beckham nchini Amerika mwisho wa msimu huu

Arsenal kumwachilia Willian ayoyomee Inter Miami inayomilikiwa na Beckham nchini Amerika mwisho wa msimu huu

Na MASHIRIKA

KIUNGO Willian Borges amefichua mipango ya kuagana na Arsenal mwishoni mwa msimu huu na kutua kambini mwa Inter Miami inayomilikiwa na mwanasoka wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, David Beckham nchini Amerika.

Willian ambaye ni raia wa Brazil alisajiliwa na Arsenal kutoka Chelsea mwishoni mwa msimu wa 2019-20 na kocha Mikel Arteta amesema kwamba atakuwa radhi kumwachilia ayoyomee Florida Kusini, Amerika baada kutoridhisha kwenye kambini mwa Arsenal jinsi ilivyotarajiwa.

Kwa mujibu wa gazeti la SunSport, kocha Phil Neville wa Inter Miami ana msukumo wa kumsajili Willian, 32, ili awe kizibo cha mwanasoka matata wa Mexico, Rodolfo Pizzaro ambaye pia ameshindwa kutamba muhula huu licha ya kuwa ndiye anayedumishwa kwa mshahara mnono zaidi kambini mwa kikosi hicho.

Ili kujinasia maarifa ya Willian ambaye atakuwa akilipwa mshahara wa hadi Sh490 milioni kwa mwaka, italazimu Inter Miami kumtia Pizzaro mnadani.

Ujira ambao Willian atakuwa akipokezwa na Inter Miami unawiana na ule ambao kwa sasa nyota wa zamani wa Juventus na Chelsea, Gonzalo Higuan anatia mfukoni katika kikosi cha Inter Miami kinachoshiriki kipute cha Major League Soccer (MLS).

Pizzaro alisajiliwa na kocha Diego Alonso na kushuka kwa makali yake kumeshuhudia nafasi yake ikitwaliwa na Federico Higuain ambaye kwa sasa anashirikiana vilivyo na Gonzalo kwenye safu ya mbele ya Inter Miami.

Maguu ya Willian naye yaliingia kutu tangu atie saini mkataba wa miaka mitatu kambini mwa Arsenal ambao kwa sasa humpokeza mshahara wa Sh30 milioni kwa wiki.

Akiwa Chelsea waliojivunia maarifa yake kwa kipindi cha miaka sita na nusu, Willian alinyanyulia kikosi hicho Kombe la FA, ubingwa wa Europa League na mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Willian atakuwa mchezaji wa tatu kuthibitisha kuondoka Arsenal mwishoni mwa msimu huu baada ya beki David Luiz na kiungo Matteo Guendouzi ambaye ataingia katika sajili rasmi ya Olympique Marseille nchini Ufaransa.

Guendouzi ambaye ni raia wa Ufaransa, amechezea Hertha Berlin kwa mkopo katika msimu huu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Umuhimu wa divai nyekundu kwenye ngozi na nywele

Leeds United wazamisha chombo cha Southampton