Arsenal kusajili Gabriel Jesus wa Man-City ili kuziba pengo la Lacazette aliyerejea Lyon

Arsenal kusajili Gabriel Jesus wa Man-City ili kuziba pengo la Lacazette aliyerejea Lyon

Na MASHIRIKA

ARSENAL wanatarajiwa kukamilisha uhamisho wa Gabriel Jesus chini ya siku saba zijazo katika hatua itakayoshuhudia fowadi huyo raia wa Brazil akiungana upya na Mikel Arteta aliyewahi kuwa msaidizi wa kocha Pep Guardiola kambini mwa Manchester City.

The Gunners wana kiu ya kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza tangu 2017 na wamekubali kuweka mezani Sh6.6 bilioni kwa ajili ya Jesus aliyekuwa pia akiviziwa na Chelsea na Tottenham Hotspur.

Jesus, 25, atakuwa sogora wa pili wa haiba kutua ugani Emirates baada ya Fabio Vieira kuagana na FC Porto ya Ureno kwa Sh5 bilioni. Arsenal wamemtwaa pia fowadi chipukizi raia wa Brazil, Marquinhos, aliyebanduka kambini mwa Sao Paulo kwa Sh444 milioni.

Chini ya Arteta, Arsenal wanapania kutumia zaidi ya Sh20 bilioni kujisuka upya muhula huu na wanatazamiwa kutwaa wanasoka Raphinha Belloli (Leeds United), Youri Tielemans (Leicester City) na Seko Fofana (Lens) kabla ya kuelekea Amerika kwa mechi za kirafiki mwezi ujao.

Jesus atasajiliwa na Arsenal kwa mkataba wa miaka mitatu huku akitia mfukoni Sh37 milioni kwa wiki. Malipo hayo yatamfanya kuwa mchezaji anayedumishwa kwa ujira mnono zaidi ugani Emirates.

Arsenal walioambulia nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2021-22, walisalia bila mshambuliaji mzoefu baada ya Alexandre Lacazette kurejea Olympique Lyon ya Ufaransa naye Pierre-Emerick Aubameyang kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona.

Kutua kwa Jesus ugani Emirates kunatarajiwa kuimarisha zaidi safu ya mbele ya Arsenal inayojivunia huduma za Bukayo Saka, Gabriel Martinelli na Eddie Nketiah ambaye ametia saini kandarasi mpya ya miaka mitano.

“Jesus ni mchezaji wa haiba kubwa anayehitaji kuwajibishwa mara kwa mara ili uwezo na utajiri wa kipaji chake ugani udhihirike. Amekosa nafasi hiyo chini ya Guardiola kambini mwa Man-City. Sasa atafungia Arsenal mabao mengi yatakayomwaminisha zaidi na kumweka miongoni mwa wavamizi bora duniani,” akasema nyota wa zamani wa Brazil, Ze Roberto.

Jesus amefunga jumla ya mabao 58 na kuchangia mengine 29 katika EPL tangu ajiunge na Man-City mnamo 2016-17 kutoka Palmeiras ya Brazil. Mbali na kunyanyua Kombe la FA na mataji matatu ya League Cup, alisaidia Man-City kuzoa ubingwa wa EPL mara nne chini ya Guardiola.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

KINYANG’ANYIRO 2022: Kaunti ya Kakamega

Man-City wang’oa Kalvin Phillips kambini mwa Leeds...

T L