Michezo

Arsenal kuwawasilishia Lyon ofa bora zaidi kwa minajili ya kiungo Aouar

September 27th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

ARSENAL wanajiandaa kuwasilisha ofa mpya ya Sh5.1 bilioni kwa minajili ya kushawishi Olympique Lyon ya Ufaransa kumwachilia kiungo Houssem Aouar, 22, kutua ugani Emirates muhula huu.

Jean-Michel Aulas ambaye ni rais wa Lyon, amethibitisha kwamba kikosi chake kilikataa ofa ya awali ya Sh4.5 bilioni iliyowekwa mezani na Arsenal.

Kwa mujibu wa Aulas, usimamizi wa Lyon unataka Arsenal iwape Sh5.6 bilioni ili kurasimisha makubaliano ya awali kisha kuwaongezea Sh1.3 bilioni mwishoni mwa muhula huu iwapo Mfaransa huyo atawasaidia kufuzu kwa gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao wa 2021-22.

Matamashi ya Aulas yanathibitisha kwamba Lyon wako tayari kumtia Aouar mnadani ila kwa masharti ambayo usimamizi umetoa kwa mnunuzi atakayejitokeza kuwania huduma za sogora huyo.

“Arsenal wangali mbali sana kufikia bei ambayo tumetangaza kwa minajili ya uhamisho wa Aouar. Iwapo kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta hakitatimiza masharti yetu, basi Aouar atasalia nasi na atakuwa nguzo ya kutuwezesha kukisuka upya kikosi chetu kwa minajili ya kampeni zijazo katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA),” akasema Aulas.

Hadi kufikia Jumamosi ambapo Arsenal walijitokeza kuwa kikosi kilichopo mstari wa mbele kuwania maarifa ya Aouar, Lyon walikuwa wameshikilia kwamba beki ya kiungo huyo ni Sh7.7 bilioni.

Hata hivyo, walishuka hadi jumla ya Sh6.9 (Sh5.6 milioni za mwanzo na Sh1.3 bilioni za baadaye) baada ya usimamizi wa Arsenal kusisitiza kwamba hazina yao ya fedha imetikiswa pakubwa na janga la corona ambalo limeathiri takriban sekta zote za maendeleo duniani.

Aouar ambaye alikuwa sehemu muhimu sana katika kampeni za Lyon kwenye UEFA msimu uliopita, amekuwa pia akimezewa mate na klabu mbalimbali maarufu barani Ulaya zikiwemo Juventus na Manchester City.

Mvutano wa bei unaozingira uhamisho wa Aouar hadi Arsenal unarejesha kumbukumbu za 2016 wakati Arsenal walipofichua azma ya kumsajili fowadi Alexandre Lacazette kutoka Lyon.

Baada ya Lyon kupandisha bei na kutoa masharti makali kuhusu uhamisho wa Lacazette wakati huo, Arsenal walizika ghafla maazimio yao kabla ya kumwendea upya mshambuliaji huyo mwaka mmoja baadaye.

Arsenal wanatarajiwa kuagana na viungo kadhaa ili kufanikisha mpango wa kusajili Aouar na Thomas Partey kutoka Atletico Madrid.

Kati ya viungo wanaotazamiwa kubanduka Arsenal ili kumruhusu Arteta kukisuka upya kikosi chake ni Lucas Torreira wa Uruguay anayehemewa na Atletico na Torino.

Arsenal wamefichua pia mpango wa kukatiza uhusiano na Sead Kolasinac, Shkodran Mustafi, Sokratis Papastathopoulos, Matteo Guendouzi na Mesut Ozil.