Michezo

Arsenal, Manchester United nari katika Uropa

September 20th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

ARSENAL ilianza Ligi ya Uropa kwa kishindo kwa kupepeta Wajerumani Eintracht Frankfurt mabao 3-0 mnamo Alhamisi, huku Mason Greenwood akisaidia Manchester United kuzima Astana ya Kazakhstan 1-0.

Nchini Ujerumani, vijana wa kocha Unai Emery, ambao msimu uliopita walifika fainali katika mashindano haya ya daraja ya pili barani Ulaya, walipata mabao mawili kutoka kwa machipukizi Joe Willock na Bukayo Saka.

Willock alipatia Arsenal uongozi katika kipindi cha kwanza alipotikisa nyavu dakika ya 38.

Dominik Kohr, ambaye timu yake ya Eintracht ilifika nusu-fainali msimu uliopita, alionyeshwa kadi nyekundu kabla ya Saka kuimarisha uongozi wa Arsenal dakika ya 85 naye mchana-nyavu matata Pierre-Emerick Aubameyang akahitimisha dakika tatu baadaye katika mechi hiyo ya Kundi F.

“Kila mtu sasa ana sababu ya kuwa na furaha. Kuendelea katika mashindano haya ni muhimu kwa hivyo ilikuwa muhimu kupata ushindi, hasa ugenini,” alisema Emery. Mechi ijayo ya Arsenal katika mashindano haya itakuwa dhidi ya Standard Liege uwanjani Emirates mnamo Oktoba 3. Wabelgiji Liege walilima Vitoria Guimaraes kutoka Ureno 2-0.

Uwanjani Old Trafford, mabingwa wa mwaka 2017 United walifunga bao lililozamisha Astana kupitia chipukizi Greenwood, 17, katika mechi ya Kundi L. Greenwood aliingia katika daftari la matukio kwa kuwa mfungaji mwenye umri mdogo kabisa wa United katika mashindano yoyote ya bara Ulaya alipoona lango zikisalia dakika 17 mechi itamatike.

Ushindi huu ni ushuhuda kuwa uamuzi wa kocha Ole Gunnar Solskjaer kufanya mabadiliko tisa kutoka timu iliyolipua Leicester City kwenye Ligi Kuu hakukosea. Aliwapa machipukizi wengi nafasi ya kuonyesha talanta zao.

“Ni kweli kuna baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza walihitaji kucheza, lakini inaridhisha tulivuna alama zote tatu,” alisema Solskjaer.

Mchuano mwingine katika kundi hili ulishuhudia AZ Alkmaar (Uholanzi) ikitoka nyuma 2-1 na kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Partizan Belgrade nchini Serbia licha ya kucheza zaidi ya saa moja watu 10 baada ya Jonas Svensson kulishwa kadi nyekundu.

Huku Arsenal na United zikifurahia kufungua mashindano kwa ushindi, Wolverhampton Wanderers kutoka Uingereza haikuwa na bahati. Ililimwa 1-0 na Braga kutoka Ureno uwanjani Molineux.

Wolves, ambayo inarejea katika mashindano ya Bara Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu 1980-1981, ilizamishwa na bao la Ricardo Horta katika mechi ya Kundi K.

Kichapo hiki kiliongeza masaibu ya Wolves, ambayo bado haijapata ushindi ligini msimu huu. Katika kundi hili, Slovan Bratislava (Slovakia) ilichabanga Besiktas (Uturuki) 4-2 jijini Bratislava.

Besiktas itaalika Wolves jijini Istanbul wiki mbili zijazo.

Mabingwa mara tano Sevilla kutoka Uhispania walichapa Qarabag (Azerbaijan) 3-0 katika kundi A. Timu 48, ambazo zimegawanywa katika makundi 12 ya timu nne, zinashiriki mashindano haya.