Arsenal na Man-United nguvu sawa ligini

Arsenal na Man-United nguvu sawa ligini

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United walipoteza fursa ya kuendeleza presha kwa wapinzani wao wakuu kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Januari 30 baada ya kulazimishiwa sare tasa na Arsenal uwanjani Emirates.

Kipa Bernd Leno wa Arsenal alifanya kazi ya ziada katika vipindi vyote viwili vya mechi na kuwanyima Edinson Cavani, Fred na Marcus Rashford nafasi za wazi ambazo vinginevyo, zingewavunia Man-United ya kocha Ole Gunnar Solskjaer ushindi muhimu wa ugenini.

Ingawa hivyo, Arsenal nao alipata nafasi nyingi za wazi kupitia kwa fowadi Alexandre Lacazette aliyeshuhudia mojawapo ya makombora yake yakigonga mwamba wa goli la Man-United.

Arsenal walikosa huduma za wachezaji Pierre-Emerick Aubameyang, Kieran Tierney na Bukayo Saka katika mchuano huo ulioshuhudia Arsenal wakimwajibisha chipukizi Martin Odegaard kwa mara ya kwanza tangu akamilishe uhamisho wake kwa mkopo kutoka Real Madrid.

Man-United walilazimika kumuondoa kiungo Scott McTominay uwanjani katika kipindi cha kwanza na nafasi yake ikatwaliwa na Anthony Martial.

Man-United kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 41, tatu nyuma ya viongozi Manchester City ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimetandazwa na Man-United. Man-City ya kocha Pep Guardiola iliwapokeza Sheffield United kichapo cha 1-0 ugani Etihad katika mechi nyingine ya Jumamosi usiku.

Huku Man-United wakiendeleza rekodi ya kutoshindwa ugenini, Arsenal nao waliendeleza rekodi ya kutopigwa ligini katika mechi saba zilizopita huku wakikosa kufungwa katika michuano mitano kati ya sita iliyopita.

Arsenal wanashikilia sasa nafasi ya nane jedwalini kwa alama 31, sita nyuma ya mabingwa watetezi Liverpool wanaofunga mduara wa nne-bora.

MATOKEO YA EPL (Januari 30):

Everton 0-2 Newcastle United

Crystal Palace 1-0 Wolves

Man-City 1-0 Sheffield Utd

West Brom 2-2 Fulham

Arsenal 0-0 Man-United

You can share this post!

Afunguka kueleza jinsi anavyoishi baada ya kutemwa

Dortmund wacharaza Augsburg na kukomesha ukame wa mechi...