Arsenal pazuri kusonga mbele kwenye Europa League baada ya kucharaza Olympiakos 3-1 katika mkondo wa kwanza wa 16-bora

Arsenal pazuri kusonga mbele kwenye Europa League baada ya kucharaza Olympiakos 3-1 katika mkondo wa kwanza wa 16-bora

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta ametaka wanasoka wake wa Arsenal kutokuwa “maadui wao wenyewe” baada ya masihara ya mabeki kuruhusu Olympiakos waliokuwa wenyeji katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Europa League kufunga bao.

Baada ya Olympiakos kusawazisha katika dakika 58 na kufuta juhudi za chipukizi Martin Odegaard aliyefungia Arsenal katika dakika ya 34, Olympiakos walijituma zaidi na kukita kambi langoni mwa wageni wao.

Nusura kikosi hicho cha Ugiriki kipate bao la pili ambalo lingezamisha kabisa matumaini ya Arsenal ya kusonga mbele kwenye Europa League msimu huu.

Hata hivyo, ililazimu masogora wa Arteta kujituma maradufu na wakafungiwa goli la pili na beki Gabriel Magalhaes katika dakika ya 79 kabla ya kiungo Mohamed Elneny kupachika wavuni goli la tatu katika mchuano huo ulioshuhudia Arsenal wakisajili ushindi wa 3-1 ugenini.

“Lazima tuwe wazi na wakweli. Tuliwapa Olympiakos nafasi tatu za wazi ambazo zingewavunia magoli ya haraka mwanzoni mwa kipindi cha pili iwapo wangezitumia vyema. Hilo lingetuacha hoi kabisa,” akatanguliza Arteta ambaye ni raia wa Uhispania.

“Walitumia mojawapo ya fursa hizo na wakasawazisha. Baada ya hapo, walitutatiza sana kwa sababu walipata nguvu ya kutaka kutuadhibu. Itatulazimu kuacha masiharaha kama hayo, yanayotusawiri kuwa maadui wetu wenyewe, iwapo tutataka kupiga hatua zaidi katika kampeni hizi za Europa League msimu huu,” akasema.

Arteta ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Everton na Arsenal, amewataka masogora wake kuwa na mazoea ya kuendea mabao ya haraka katika takriban kila mchuano badala ya kujipa presha tele katika baadhi ya mechi ambazo wana fursa za wazi za kufunga idadi kubwa ya mabao.

Beki David Luiz na kiungo Odegaard walionyesha utepetevu mkubwa kabla ya masiharaha ya kipa Bernd Leno na kiungo Dani Ceballos kuwapa Olympiakos fursa ya kufungiwa bao la kusawazisha kupitia kwa Youssef El Arabi.

Bao hilo lilionekana kuwaweka Arsenal pabaya, katika presha sawa na iliyowahi kuwapata katika michuano ya awali dhidi ya Burnley ligini na Benfica kwenye hatua ya 32-bora ya Europa League.

“Nafasi na bao ambalo Olympiakos walipata lilitokana na makosa yetu wenyewe. Ukweli ni kwamba hali hii lazima ikome na ni wajibu wangu kuongoza kikosi kufanya hivyo,” akaongeza Arteta atakayeongoza wanasoka wake kuwa wenyeji wa mchuano wa mkondo wa pili mnamo Machi 18, 2021.

Olympiakos ndio waliowabandua Arsenal kwenye hatua ya 32-bora ya Europa League katika kampeni za msimu wa 2019-20.

Mbali na Odegaard ambaye ni kiungo chipukizi anayechezea Arsenal kwa mkopo kutoka Real Madrid ya Uhispania, wanasoka wengine waliotatiza pakubwa mabeki wa Olympiakos kwenye mchuano huo wa mkondo wa kwanza ni Bukayo Saka, Willian Borges na Pierre-Emerick Aubameyang.

Kufikia sasa, Arsenal wameshinda mechi nane kati ya tisa zilizopita kwenye Europa League msimu huu. Masogora hao wa Arteta wameambulia sare mara moja pekee na ndio wanaojivunia idadi kubwa zaidi ya mabao baada ya kucheka na nyavu za wapinzani mara 27.

Arsenal kwa sasa wanajiandaa kualika Tottenham Hotspur kwenye gozi kali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Machi 14, 2021 uwanjani Emirates.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TAHARIRI: Uamuzi wa kafyu uzingatie usalama

Tottenham sasa guu moja ndani ya robo-fainali za Europa...