Michezo

Arsenal sasa majogoo wa kulazimisha sare

February 2nd, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

ARSENAL imeendelea kuvuma kama wafalme wa kugawana alama kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupiga sare yake ya 13 msimu huu ilipotoka 0-0 dhidi ya Burnley uwanjani Turf Moor, Jumapili.

Vijana wa Mikel Arteta, ambao walipoteza nafasi nyingi nzuri dhidi ya Burnley na pia kuponea chupuchupu kufungwa, sasa wameandikisha sare nne mfululizo. Waliingia mechi ya Burnley wakiwa wametoka 1-1 na Crystal Palace na Sheffield United na 2-2 dhidi ya Chelsea.

“Wanabunduki” wa Arsenal wamesalia katika nafasi ya 10 kwa alama 31 sawa na nambari 11 Burnley, ambao wako nyuma kwa sababu ya tofauti ya magoli.

Arsenal inaongoza katika timu zilizotoka sare msimu huu wa 2019-2020 baada ya kupiga sare 13 ikifuatiwa na Wolves (11), Palace na Sheffield (tisa kila mmoja) na Watford (nane) katika nafasi tano za kwanza kwenye jedwali la timu zilizopiga sare nyingi.

Liverpool inaongoza msimu kwa alama 73 baada ya kupiga Southampton 4-0 Jumamosi na kudumisha rekodi yake ya kutoshindwa ligini msimu huu kuwa 24.

Vijana wa Jurgen Klopp wamefungua mwanya wa alama 22 dhidi ya wapinzani wa karibu, mabingwa watetezi Manchester City, ambao watamenyana na nambari nane Tottenham Hotspur baadaye Jumapili usiku.