Michezo

Arsenal sasa ni 'piga ua' ikikutana na wanyonge

October 8th, 2018 2 min read

LONDON, UINGEREZA

NYOTA Aaron Ramsey alifunga mojawapo ya magoli ambayo yanatarajiwa kuwania tuzo ya bao bora la msimu huu katika ushindi mnono wa 5-0 uliosajiliwa jana na Arsenal dhidi ya Fulham katika kivumbi cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Ushindi wa Arsenal ulikuwa wao wa tisa kwa mfululizo katika kampeni za EPL tangu Aprili 2015.

Fowadi wa zamani wa Olympique Lyon, Alexandre Lacazette alipachika wavuni magoli mawili kabla ya Ramsey aliyetokea benchi kukizamisha chombo cha wenyeji wao baada ya Pierre-Emerick Aubameyang kutikisa pia nyavu za wapinzani wao mara mbili.

Lacazette alifungua ukurasa wa mabao katika uwanja wa Craven Cottage kunako dakika ya 29 baada ya kushirikiana vilivyo na beki mzawa wa Uhispania, Nacho Monreal na kumwacha hoi kipa Marcus Bettinelli.

Japo bao hilo lilitarajiwa kuyazima makali ya Fulham waliopania kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani, mambo yalikuwa kinyume. Luciano Vietto aliwasawazishia waajiri wake mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kushirikiana ipasavyo na Mjerumani Andre Schurrle aliyempiku Monreal kimaarifa kisha kumsaza kipa Bernd Leno akitapatapa.

Arsenal walirejelea kampeni za kipindi cha pili kwa hamasa na ghera tele huku Bettinelli akilazimika kufanya kazi nyingi za ziada kuyapangua makombora mazito aliyoelekezewa na Lacazette kisha beki Hector Bellerin.

Ramsey ambaye ni mzawa wa Wales aliingia ugani kunako dakika ya 67 na kupachika wavuni bao la tatu la Arsenal sekunde 39 baadaye. Hii ilikuwa baada ya Lacazette kutikisa nyavu za Fulham kunako dakika ya 49. Kikosi hicho kilirejea pamoja na Wolves na Cardiff City kunogesha kampeni za EPL msimu huu.

Aubameyang aliwafungia Arsenal bao la nne katika dakika ya 79 baada ya kukamilisha kwa ustadi mkubwa krosi aliyomegewa na Bellerin.

Nyota huyo mzawa wa Gabon alikizamisha kabisa chombo cha Fulham mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kushirikiana vyema na Ramsey katika dakika ya 90.

Fulham walipata nafasi kadhaa za kurejea mchezoni kupitia kwa Aboubakar Kamara, ila wakazidiwa maarifa katika takriban kila idara. Nusura nyota huyo mzawa wa Ufaransa atikise nyavu za Arsenal mwishoni mwa kipindi cha pili ila akapaisha mpira aliopokezwa na Cyrus Christie.

Ushindi wa Arsenal ambao ulikuwa wao wa sita mfululizo katika EPL msimu huu uliwapandisha hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 18 sawa na watani wao wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur ambao wana mabao machache.

Hapo jana, vita vya kuwania nafasi ndani ya mduara wan ne-bora katika kipute cha EPL msimu huu vilionekana kuchacha zaidi wakati Liverpool walipokuwa wakiwaalika Manchester City uwanjani Anfield nao Chelsea wakipepetana na Southampton katika uwanja wa St Mary’s.

Fulham kwa sasa wanasalia katika nafasi ya 17 jedwalini kwa alama tano, mbili pekee mbele ya Huddersfield. Newcastle United na Cardiff City wanakokota nanga mkiani mwa jedwali kwa alama mbili kila mmoja.

Baada ya kupoteza michuano miwili ya ufunguzi katika kampeni za EPL msimu huu dhidi ya Man-City na Chelsea, Arsenal wanaonesha kila dalili ya kupata uthabiti chini ya kocha mpya Unai Emery aliyemrithi Arsene Wenger mwishoni mwa msimu jana.

Ni matarajio ya kocha huyo kwamba uhusiano bora kati ya Aubameyang na Lacazette ndani nan je ya uwanja utakitambisha kikosi chake hata zaidi katika kampeni za msimu huu ili hatimaye kiweze kuwa tishio hata machoni mwa wapinzani wao wakuu ligini na katika soka ya bara Ulaya.

Ramsey na Aubameyang waliingia katika mabuku ya historia kwa kuwa wachezaji wawili wa kwanza katika historia ya EPL kutokea benchi na kufunga bao na kuchangia jingine katika mchuano mmoja.

 

MATOKEO YA EPL RAUNDI YA 8

Burnley 1-1 Huddersfield

Watford 0-4 Bournemouth

Tottenham 1-0 Cardiff

Brighton 1-0 West Ham

Palace 0-1 Wolves

Leicester 1-2 Everton

Man-Utd 3-2 Newcastle

Fulham 1-5 Arsenal

Southampton 0 -3 Chelsea

Liverpool 0-0 Man-City