Arsenal wacharaza Burnley na kupunguzia Arteta presha ya kupigwa kalamu

Arsenal wacharaza Burnley na kupunguzia Arteta presha ya kupigwa kalamu

Na MASHIRIKA

MARTIN Odegaard alifunga bao kupitia mpira wa ikabu na kusaidia waajiri wake Arsenal kukung’uta Burnley 1-0 na hivyo kusajili ushindi wao wa kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Odegaard ambaye ni raia wa Norway, aliaminiwa fursa ya kupiga mpira huo wa ikabu baada ya Ashley Westwood kumchezea visivyo kiungo Bukayo Saka hatua chache nje ya kijisanduku.

Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa Odegaard kufungia Arsenal tangu apokezwe mkataba wa kudumu na kikosi hicho kutoka Real Madrid ya Uhispania kwa Sh4.7 bilioni.

Burnley walinyimwa nafasi maridhawa ya kusawazisha mambo kupitia penalti baada ya refa Anthony Taylor kubatilisha maamuzi yake aliporejelea teknolojia ya VAR kubaini iwapo kipa Aaron Ramsdale alikuwa amemchezea visivyo Matej Vydra.

Burnley walikuwa wakisakata mchuano huo mbele ya mashabiki wao wa nyumbani siku chache baada ya mkufunzi wao Sean Dyche kupokezwa mkataba mpya wa miaka minne. Mechi hiyo iliwapa Burnley jukwaa la kumwajibisha fowadi Maxwel Cornet wa Ivory Coast kwa mara ya kwanza.

Ushindi huo ambao ulikuwa wa pili mfululizo kwa Arsenal msimu huu, ulimpunguzia kocha Mikel Arteta presha kubwa ya kutimuliwa ikizingatiwa kwamba kwa sasa wako ndani ya orodha ya 10-bora.

Kwa upande wao, Burnley wanashikilia nafasi ya pili kutoka mwisho kwa alama moja pekee kutokana na mechi tano za ufunguzi wa msimu huu.Arsenal walishuka dimbani kuvaana na Burnley wakitawaliwa na motisha ya kuendeleza ubabe na rekodi ya kutoshindwa ugani Turf Moor tangu 1973.

Burnley walikosa makali dhidi ya Arsenal na walionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara hadi dakika ya 57 ambapo Cornet aliletwa uwanjani.Ushirikiano mkubwa kati ya Odegaard, Emile Smith Rowe na Thomas Partey ulichangia pakubwa uthabiti wa Arsenal katika safu ya kati japo watatu hao walishindwa kuwaandalia mafowadi Nicolas Pepe na Pierre-Emerick Aubameyang nafasi nyingi za wazi.

Akiwa na umri wa miaka 22 pekee, Odegaard angali na muda mrefu wa kudhihirishia mashabiki sababu kuu zilizowachochea Real Madrid kumnunua akiwa na umri wa miaka 16 mnamo Januari 2015.

Ingawa aliwajibikia Real mara 11 pekee, Odegaard amekuwa akiimarika mara kwa mara.

  • Tags

You can share this post!

Man-City wapoteza pointi mbili muhimu za EPL dhidi ya...

Wakenya wamiminika UG kununua mafuta