Arsenal wacharaza Crystal Palace ugenini na kupaa hadi nafasi ya tisa kwenye jedwali la EPL

Arsenal wacharaza Crystal Palace ugenini na kupaa hadi nafasi ya tisa kwenye jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Roy Hodgson amesema kibarua cha kunoa Crystal Palace kimekuwa sawa na “hadithi au safari ya kuridhisha” licha ya mchuano wake wa mwisho ugani Selhurst Park kukamilika kwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Arsenal mnamo Mei 19, 2021.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal walifunga mabao mawili katika dakika za mwisho na kuzamisha chombo cha Palace ambao wataagana rasmi na Hodgson mwishoni mwa msimu huu. Hodgson, 73, atakatiza uhusiano wake na Palace baada ya kudhibiti mikoba ya kikosi hicho kwa kipindi cha miaka minne.

Nicolas Pepe alifungulia Arsenal karamu ya mabao katika dakika ya 35 kabla ya kufunga jingine sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki 6,500 kupulizwa.

Awali, Palace walikuwa wamesawazishiwa na Christian Benteke katika dakika ya 62 kabla ya chipukizi Gabriel Martinelli kuwarejesha Arsenal mchezoni alipokamilisha krosi ya Martin Odegaard katika dakika ya 90. Bao la Benteke lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Andros Townsend.

Palace huenda wakakamilisha kampeni za EPL msimu huu katika nafasi ya 12 iwapo Manchester United watawachabanga Wolves uwanjani Molineux mnamo Mei 23, 2021. Palace ambao watapepetana na Liverpool katika mchuano wao wa mwisho wa msimu sasa wanakamata nafasi ya 13 kwa alama 44.

Hodgson ndiye kocha mkongwe zaidi kuwahi kudhibiti mikoba ya kikosi kinachoshiriki gozi la EPL. Tangu akitwae chombo cha kikosi hicho mnamo Septemba 2017, amewaongoza waajiri wake kuepuka kushuka ngazi baada ya kuambulia nafasi za 11, 12 na 14 mtawalia.

Mwishoni mwa mechi, Hodgson ambaye pia amewahi kunoa timu ya taifa ya Uingereza, aliandaliwa gwaride la heshima na wanasoka wa pande zote mbili – Palace na Arsenal.

Licha ya kushinda Palace, matumaini ya Arsenal ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya orodha ya sita-bora jedwalini na kufuzu moja kwa moja kwa Europa League muhula ujao yalizamishwa na West Ham United waliopiga West Brom 3-1 ugani The Hawthorns.

Arsenal ambao wamepoteza jumla ya mechi 13 muhua huu, kwa sasa wanashikilia nafasi ya tisa kwa alama 58, nne nyuma ya West Ham wanaokamata nambari ya sita.

Ufufuo wa makali ya Arsenal katika wiki chache zilizopita umewashuhudia wakisajili ushindi wa nne mfululizo ligini kwa mara ya kwanza tangu 2018. Watakamilisha kampeni za msimu huu dhidi ya Brighton mnamo Mei 23 uwanjani Emirates.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Adai kortini akivuta bangi huongeza nguvu za kiume

Wachomea Rais picha