Michezo

Arsenal waendeleza masaibu ya Sheffield United kwenye EPL

October 5th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ARSENAL walifunga mabao mawili ya haraka na kuendeleza masaibu ya Sheffield United ambao hawana alama yoyote katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hadi kufikia sasa.

Arsenal walifufua makali yao kwenye mchuano huo uliochezewa ugani Emirates katika dakika ya 60 kupitia kwa bao la chipukizi Bukayo Saka aliyeshirikiana na beki Hector Bellerin.

Dakika tatu baadaye, vijana wa kocha Mikel Arteta walifunga bao la pili kupitia kwa Nicolas Pepe aliyetokea benchi katika kipindi cha pili na kukamilisha pasi 19.

Arsenal walionekana kutamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira hadi dakika ya 83 ambapo David McGoldrick alitikisa nyavu za wenyeji wao na kufungia Sheffield United bao la kwanza msimu huu.

Japo goli hilo lilionekana kuwarejesha Sheffield United mchezoni, halikutosha kutikisa uthabiti wa Arsenal walioleta ugani beki Ainsley Maitland-Niles mwishoni mwa kipindi cha pili.

Sheffield United kwa sasa wamepoteza jumla ya mechi saba mfululizo za EPL kwa mara ya kwanza tangu 1975.

Arsenal kwa sasa wanajivunia alama sita kutokana na mechi tatu za EPL baada ya kupokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa mabingwa watetezi Liverpool mnamo Septemba 28, 2020.

Japo matokeo ya Arsenal hayakuwa bora zaidi jinsi yalivyotarajiwa, miamba hao wa zamani wa soka ya Uingereza walisajili ushindi wa nne kutokana na mechi nne za mashindano yote dhidi ya wapinzani wao isipokuwa Liverpool.

Nusura Arsenal wasalie uwanjani na wachezaji 10 pekee katika kipindi cha kwanza baada ya beki David Luiz kumkabili visivyo fowadi Oliver Burke aliyemfanyia kipa Bernd Leno kazi ya ziada.

Ilikuwa hadi dakika ya 28 ambapo Arsenal walifanya jaribio la kwanza langoni pa Sheffield United kupitia kwa fowadi Eddie Nketiah aliyeondolewa ugani katika kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Pepe.

Makombora mawili ya fowadi na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang langoni pa Sheffield United yalidhibitiwa vilivyo na kipa Aaron Ramsdale mwishoni mwa kipindi cha pili. Aubameyang alichezewa visivyo na kiungo Sander Berge mwishoni mwa kipindi cha kwanza.