Michezo

Arsenal waingia sokoni kutafuta kipa baada ya ligi kuwaponyoka

May 24th, 2024 1 min read

GEOFFREY ANENE Na MASHIRIKA

ARSENAL FC wanaaminika kuwa sokoni kutafuta kipa wakati huu Mwingereza Aaron Ramsdale anaonekana anaelekea kuondoka uga wa Emirates baada ya kupoteza nafasi yake kama kipa nambari moja.

Soko litafunguliwa Juni 14 hadi Septemba 2, 2024.

Taarifa nchini Uholanzi zinadai kuwa Wanabunduki hao ambao walitumia Mhispania David Raya kwa kipindi kikubwa cha msimu 2023-2024 kwa mkopo kutoka Brentford, sasa wanasemekana kummezea mate Justin Bijlow.

Kipa huyo Mholanzi mwenye umri wa miaka 26 anachezea Feyenoord. Kuwasili kwa Raya,28, kutoka Brentford kulisababisha Ramsdale,26, kupoteza nafasi yake, huku kocha Mikel Arteta akimwamini Raya zaidi michumani.

Inaaminika Arsenal watalenga kununua kabisa Raya na pia kutafuta kipa atakayempa ushindani.

Gumzo linadai kuwa Liverpool pia wametuma maskauti kumtazama Bijlow, 26, aliyedakia Feyenoord mara 17 kwenye Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie). Katika idadi hiyo ya mechi, Bijlow hajafungwa bao katika michuano minane.